KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameipogeza Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameyataja maeneo matatu ambayo UWT inafanya kazi kuwa ni kuandikisha wanachama wapya, kuhimiza wanachama kulipa ada na kubuni miradi ya kiuchumi.
Chongolo alitoa pongezi hizo, alipokuwa mgeni rasmi katika kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kilichofanyika Makao Makuu ya Chama Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Chongolo, maeneo hayo matatu kwa CCM ni muhimu sana, kwa kuwa bila hayo hakuna Chama wala Jumuiya.
“Kwani bila kuingiza wanachama wapya maana yake waliopo wataendelea kupungua, bila kuwa na msingi imara wa uchumi, Jumuiya itakuwa omba omba na bila kujenga uhai wa Jumuiya hatutakuwa na Jumuiya imara na yenye nguvu ya kusimamia maslahi ya wanawake nchini,” alisisitiza.
Jumuiya hiyo kwa kupitia Mwenyekiti wake Taifa, Gaudentia Kabaka, imetoa tamko la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuuunda kamati maalumu ya kumshauri kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia, ambapo itasaidia kutimiza malengo ya hamsini kwa hamsini.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Thuwaiba Kisasi, alisema wanawake wataendelea kusimama kidete katika kusimamia maslahi ya wanawake wote nchini na ya Chama Cha Mapinduzi.
NA MWANDISHI WETU, DODOMA