KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amemtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, kufika mkoani Kagera mara moja kutatua changamoto za upatikanaji wa maji ikiwemo ya baadhi ya miradi kutoanza kutoa huduma hiyo.
Agizo lake linatokana na ripoti za baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya CCM, kubaini changamoto ya kusuasua baadhi ya miradi waliyoitembelea wakiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na uimara wa Chama.
Chongolo aliyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara aliyoiongoza ya wajumbe wa Sekretarieti ya CCM mkoani Kagera.
“Katika ripoti za wajumbe wa Sekretarieti zilizowasilishwa hapa, zipo baadhi zimetaja changamoto ya maji ikiwemo miradi kuwa na harufu ya kuhujumiwa. Namuagiza Waziri wa Maji (Aweso), afike hapa mara moja.
“Suala la maji halipaswi kufanyiwa mzaha. kama kuna watu wamehujumu miradi hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Chongolo.
ALICHOBAINI SHAKA
Kauli ya Chongolo inatokana na ripoti ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ya kubaini harufu ya hujuma katika mradi wa maji wa Katale katika Halmashauri ya Wilaya Bukoba.
Awali akiwa katika ziara hiyo wilayani Bukoba, Shaka alifika Kijiji cha Katale ulipo mradi huo uliogharimu zaidi ya sh. milioni 590 na kukuta haufanyikazi mbali na kukamilika na kukabidhiwa kwa kijiji hicho.
Shaka alitoa siku 30 kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machari kuwasilisha ripoti ya uchunguzi wa mradi huo na hatua zichukuliwe.
MAAGIZO MENGINE YA CHONGOLO
Kupitia kikao hicho, Chongolo aliwataka wana CCM mkoani Kagera, kuendelea kushikamana na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Chongolo aliwataka wana CCM kuacha majungu, fitina na kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Pia alipongeza kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya elimu, afya na miundombinu.
Na MWANDISHI WETU, Bukoba