KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amekubali ombi la viongozi wa Mkoa wa Katavi, kuuwezesha mkoa huo kuwa na vihenge na maghala ya kanda ya kuhifadhia mahindi.
Chongolo alipokea maombi hayo baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Mwanamvua Mrindoko, kutoa ombi hilo kwa CCM, ili kuhimiza wizara kuidhinisha kwa haraka maombi hayo, yatakayosaidia kusogeza karibu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Aidha, Chongolo aliitaka NFRA, kuanza kutafsiri kwa vitendo namna miradi hiyo ya ujenzi wa maghala inavyoleta matokeo chanya, kwa sababu haitakuwa busara kuwa na vihenge, baada ya muda wananchi walalamikie masoko ya kuuza mahindi au mazao yao.
“Ni lazima kuweka mpango mapema wa kununua na kuhifadhi mahindi na si kusubiri mpaka muda unapofika mwisho ndio mnaanza kukimbizana,” alisema.
Mkuu wa mkoa huo, Mwanamvua akizungumza kuhusu mradi huo, alisema mpaka kufikia Machi mwakani, vihenge hivyo vitakuwa tayari vimeanza kufanya kazi.
Alisema mradi huo wa vihenge sita vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 3,300 kila kimoja, sawa na tani 20,000 ulianza kujengwa Januari 14, 2019 na unatarajiwa kukamilika Machi 31, mwaka 2022 kwa gharama ya sh. bilioni 14.
Pia aliongeza kuwa mpaka sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 95 kwa vihenge na asilimia 80 miundombinu mingine.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Chongolo alisisitiza matumizi mazuri ya fedha za ndani za halmashauri, ambapo alisema ni lazima zisimamiwe ipasavyo ili zilete matokeo chanya ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kama ilivyotarajiwa.
Alisema amefurahishwa na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Nsemurwa, ambacho kinajengwa kwa kutumia mapato ya ndani, huku ujenzi ukienda kwa kasi na kwa ubora.
Chongolo alieleza hayo, baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa kwa kutumia mapato ya ndani kwa gharama ya sh. milioni 400 na kutarajiwa kukamilika Februari, mwakani.
Na MWANDSIHI WETU