KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameutaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuweka mapema mpango wa kuhakikisha ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima unafanyika kwa wakati.
Alitoa maagizo hayo alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa ghala na vihenge sita vya kuhifadhia mazao ya wakulima Kanda ya Sumbawanga, wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi.
Chongolo alisema ni lazima NFRA ianze kutafsiri kwa vitendo namna miradi ya ujenzi wa maghala na vihenge itakavyoleta matokeo chanya, huku akisema haitakuwa busara kuwepo na vihenge halafu baadaye wakulima waanze kulalamika mahala kwa kuuza mazao yao.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, alimweleza Katibu Mkuu Chongolo kuwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani na kuanza kufanya kazi.
Mradi huo wa vihenge sita vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 3,300 kwa kila kimoja, ulianza kujengwa Januari 14, 2019 na unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani.
Awali, katika taarifa ya NFRA Kanda ya Sumbawanga, ilieleza kuwa, mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 14, tayari umetekelezwa kwa asilimia 95 kwa ujenzi wa vihenge na asilimia 80 ujenzi wa miundombinu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alimuomba Chongolo kusaidia kusukuma maombi yao kwa serikali kupitia wizara ya kilimo, kuidhinisha ombi la kuifanya Katavi kuwa Kanda ya Ununuzi wa Mazao ya NFRA.
Mwanamvua alimweleza Katibu Mkuu kuwa, mpango huo utasaidia wakulima wa Katavi kupata huduma ya kuuza mazao yao kwa NFRA kwa ukubwa na kwamba NFRA itakuwa karibu zaidi tofauti na ilivyo sasa.
Alisema kuwa uzalishaji wa mahindi na mazao mengine Katavi ni mkubwa na kwamba mkoa huo unafunguka kwa kasi kibiashara na kiuchumi.
Kufuatia ombi hilo, Chongolo alikubali na kuahidi kuwasilisha kwa serikali ili kuidhinisha maombi ya viongozi wa mkoa kufanya Katavi kuwa kanda kwa ajili ya ununuzi na uhifadhi wa mazao ya mahindi.
Katika hatua nyingine, Chongolo alisema ni lazima halmashauri zisimamie matumizi mazuri ya fedha za ndani ili zilete matokeo chanya kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Katibu Mkuu alieleza kufurahishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha Afya cha Nsemurwa wilayani Mpanda, ambacho kinajengwa kwa kutumia mapato ya ndani.
Alitoa kauli hiyo alipotembelea na kukagua ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa kwa kutumia mapato ya ndani kwa gharama ya sh. milioni 400 kilichoanza Septemba 8, mwaka huu na kinatarajiwa kukamilika Februari, mwakani.
Na MWANDISHI WETU, Mpanda