KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema malengo ya kuanzisha Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), hayakuwa na maana ya kuwatumia vijana hao katika utafutaji wa kura za wagombea au kuhangaika na masuala binafsi ya viongozi bali ni kujenga nchi kwa kujitolea.
Pia, amesema umefika wakati kwa vijana wa UVCCM kujitokeza kwa wingi kukipigania Chama na serikali na kuwataka viongozi wa mikoa na wilaya kutumia Umoja huo, kujenga miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo wanayoianzisha katika maeneo au inayojengwa na serikali.
Chongolo alitoa maagizo hayo, baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa ambavyo vinajengwa kwa nguvu ya UVCCM, katika Shule ya Bukama, Kata ya Kagoma wilayani Muleba, mkoani Kagera, ambapo alisema anawapongeza vijana walioshiriki ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.
Alisema malengo ya Chama kuanzisha umoja huo ni kujenga nchi kwa kujitolea na baadaye kupata fursa ya kwenda kulitumikia taifa kwa faida yao na nchi kutokana na kujengwa katika falsafa nzuri na zenye kujenga maadili na kulinda uzalendo wa nchi hususan katika kuleta maendeleo.
Katibu Mkuu Chongolo alisema miaka ya nyuma kazi ya umoja wa vijana ilikuwa kujitolea kujenga miundombinu na kufanya mambo mengine ya maendeleo na baadaye kupata fursa ya kwenda jeshini kulitumikia taifa kwa faida yao na nchi kwa ujumla, hivyo ni wakati mwafaka wa vijana kutambua malengo hayo.
“Miaka ya 2000 kwenda nyuma, asilimia 90 ya vijana ambao walikuwa wanachukuliwa kwenda jeshini, walikuwa wanatokana na umoja wa vijana na ni kwa sababu walikuwa wanajitolea kulitumika taifa kwa kupitia umoja huo,” alisema.
Alisema kwa sasa vijana wengi wa umoja wa vijana wamekuwa wapambe namba moja wa wagombea na wahangaikaji wa mambo binafsi ya viongozi, huku wakiacha majukumu yao halisi.
Katika hatua nyingine, Chongolo aliipongeza UVCCM Wilaya ya Muleba, kwa kujitolea kujenga vyumba vya madarasa, huku akiwataka viongozi wa halmashauri hiyo na mkoa mzima, kuendelea kuwatumia vijana hao kujenga miundombinu mingine kwani wameonyesha utayari na uwezo wa kufanya kazi hiyo kwa moyo.
Na MWANDISHI WETU, Muleba