WAKAZI wa Kijiji cha Kakulungu, Kata ya Milambo-Itobo wilayani Nzega mkoani Tabora, wamekumbwa na taharuki baada ya chui kuvamia kijijini hapo na kuua mtoto wa miaka 11 kisha kujeruhi wananchi wengine nane.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, ACP Richard Abwao, amethibitisha kutokea tukio hilo ambapo alibainisha kuwa mtoto aliyeuawa kuwa ni Maganga Myete (11) mkazi wa Kijiji hicho.
Amesema chui huyo ambaye alitokea katika Hifadhi ya Msitu wa Ipala, alivamia makazi ya watu saa mbili usiku kwa kumshambulia mtoto huyo katika maeneo mbalimbali ya mwili kwa kumng’ata shingoni ambako alitokwa damu nyingi na kupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitalini.
Abwao aliongeza kuwa baada ya kumshambulia mtoto, chui huyo aliendelea kujeruhi watu wengine katika maeneo mbalimbali na kuwasababishia majeraha kisha kutoweka.
Alieleza kuwa baada ya kutoweka chuo huyo walifanya msako kwa kushirikiana na wananchi na maofisa wanyamapori na kufanikiwa kumuua.
Kamanda Abwao alitaja watu waliojeruhiwa kuwa ni Peter Ziloba (55) Juma Seleman (78) Jumanne Yona (29) Hadija Mrisho (20) na mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kahurungu, Buhere Emanuel (11) wote wakazi wa Kijiji cha Magengati.
Wengine waliojeruhiwa ni Lusia Ilumba (70) Mateo Lubigiri (60) na Mwashi Bundala (10) ambao ni wakulima wanaoishi katika Kijiji cha Milambo-Itobo.
Aliongeza kuwa majeruhi wote wamepelekwa katika Hospitali ya Ndala wilayani humo kwa ajili ya matibabu zaidi na afya zao zilikuwa zinaendelea vizuri.
Alitoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya misitu ya hifadhi kujihadhari dhidi ya wanyama wakali ikiwemo kutoacha watoto pekee yao na pindi wanapowaona wanyama katika makazi yao watoe taarifa.
NA ALLAN KITWE, Nzega