KATIBU Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif, amesema kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa walimu na uwepo wa kizazi cha dijitali, ndiyo sababu ya serikali kuamua kutumia migambo na askari polisi wenye silaha, kuwasimamia walimu wanapotekeleza majukumu ya usimamizi wa mitihani.
Vilevile amesema hali hiyo imesababishwa na kushamiri kwa vitendo vya wizi wa mitihani na kwamba itafika wakati, watapelekewa Jeshi la Wananchi (JWTZ), kuwasimamia, jambo ambalo ni la aibu kwa kada hiyo ya ualimu.
“Ni lazima wabadilishe tabia na miendo yao na kurejesha nidhamu, kama ilivyokuwa miaka ya 80 ambapo mitihani ilisimamiwa na walimu pekee,” amesema.
Katibu huyo ametoa kauli hiyo, jijini Dodoma, kwenye kongamano la Chama Cha Walimu Wanafunzi, Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOSTA), tukio lililoambatana na mahafali ya wanafunzi walimu tarajali 232 wa mwaka wa tatu chuoni hapo.
Amesema kitendo cha walimu kukosa uamini ni kuvunja maadili na kuitia doa kada ya Ualimu nchini, huku akiwataka walimu kubadilika na kurejea kwenye miiko ya ualimu na kuachana na tabia ya wizi wa mitihani, uliosababisha walimu kupelekewa migambo na askari kwenye vyumba vya mitihani.
“Hatujachelewa muda bado upo tubadilike, turejee kwenye miiko yetu kama tulivyojifunza vyuoni, tutambue kuwa vitendo hivyo pia vimekuwa vikiwanyima haki watoto kutokana na kuingia hofu wanapoona chumba cha mitihani wamesimamiwa na askari kwenye silaha au mgambo.
“Tuache jamani, tuwe kama walimu wa miaka 80 ambao walikuwa waaminifu na jukumu la mitihani walisimamia wenyewe,” amesema Deus.
Akizungumzia ajira za walimu, amesema mwaka jana walimuomba Dk. John Magufuli, ajira za walimu ambapo alikubali ombi hilo na ndio ulikuwa msingi wa nafasi zaidi ya 6,000 kutangazwa na serikali hivi karibuni.
Katibu mkuu huyo amesema CWT itaendelea kuwasilisha ombi la ajira mpya za walimu kwa serikali kila inapopata nafasi ya kukutana na viongozi.
Na Happiness Mtweve