KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amekerwa na danadana zinazoendelea kupata utatuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa eneo la kiwanja cha ndege mkoani Mtwara na mamlaka ya viwanja vya ndege.
Shaka aliyasema hayo alipotembelea eneo hilo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa mwaka jana.
Alisema kwamba, danadana hizo hazina tija kwa wananchi na kutoa maelekezo kwa wizara nne kukutana haraka ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
“Ndugu zangu mimi nilisema nije, kuja kwangu ni kuweka msisitizo kwamba, Chama kinafuatilia kwa karibu sana mgogoro huu kati ya wananchi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na mamlaka nyingine ambazo zimeingia katika kadhia hii.
“Kama kuna upande una haki, kama kuna upande hauna haki, lakini unahitaji huruma, basi mamlaka zinazokaa zikae na zipime, zitafakari uzito wa kuusaidia huo upande na athari endapo watausaidia huo upande ni zipi na mwisho, waje na majibu ili wananchi hawa waishi kwa amani.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na ninyi katika kuhakikisha mgogoro huu unafikia mwisho,” alisema.
Alisema wizara nne zinahusika katika utatuzi wa mgogoro huo, hivyo ameziagiza kukutana haraka ili kuutafutia ufumbuzi.
“Ukifuatilia hapa, kuna karibu wizara tatu zinaingia kwa nne. Wizara ya Uchukuzi ambao ndio wana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Wizara ya Nishati ambao wao wana dhamana ya gesi.
“Wizara ya TAMISEMI ambao wao wana watu na Wizara ya Ardhi ambao wamepewa mamlaka ya kisheria kusimamia mambo ya ardhi…Sasa taasisi moja inapokuwa mlalamikaji kwamba wenzake hawapo tayari kutoa ushirikiano ni jambo linalosikitisha ndugu zangu.
“Maelekezo ya Chama ni kwamba, taasisi hizo nne nilizozitaja zikutane haraka kujadili kadhia hii na waje na majibu ya kuwapa wananchi,” ameagiza.
Shaka ametoa agizo hilo baada ya Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa wa Mtwara, Samuel Miruma kusema kusuasua kwa utatuzi wa mgogoro huo, kunachangiwa na baadhi ya taasisi zinazohusika kuchelwa kutoa ushirikiano.
Meneja huyo alisema tayari wananchi 100 wakazi wa Mtaa wa Mangamba, Kata ya Mtawanya wamelipwa fidia zao.
APOKEA TUZO YA RAIS SAMIA
Katika hatua nyingine, Shaka alipokea tuzo maalumu iliyotolewa na wanawake mkoani Mtwara kwa Rais Samia kwa kutambua mchango wa kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo hususan mkoani humo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Shaka alisema tuzo hiyo itamtia moyo na kumpa ari Rais Samia katika kuwatumikia Watanzania.
Kitendo cha kumpatia tuzo mnamtia moyo, mnapa ari ya kuwatumikia Watanzania, lakini mnamtia ari ya kutimiza malengo yenu akinamama katika mambo muhimu kama ambavyo nimesema.
“Wito wangu kwenu, msisite, msiishie hapa endeleeni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu, kila mmoja kwa imani yake Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema ili aweze kututumikia Watanzania,” alisema.
Shaka alisema aliyoyafanya Rais Samia, wanawake wanayajua hata ukiwaamsha usingizini wanakwambia ameifungua Mtwara.
Awali, akizungumza kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, kwa niaba ya wanawake hao Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Mtwara, Zuhura Farid, alisema kwa niaba ya wanawake wengine wote, wanampongeza Rais Samia kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya.
Na SOPHIA NYULUSI, Mtwara