SERIKALI imesema hivi karibuni itatangaza zabuni ya kumpata mkandarasi wa kujenga daraja eneo la Jangwani, jijini Dar es Salaam, ambalo linasababisha changamoto ya usafiri kwa wananchi nyakati za mvua.
Pia, imesema Daraja la Selander (Tanzanite) lenye urefu wa kilomita 1.03 na barabara unganishi kilomita 5.2 ambalo hadi kukamilika kwake imetumika sh.bilioni 243, linatarajiwa kuzinduliwa kesho, Februari 1, 2022.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameeleza kuwa magari yataruhusiwa kupita katika Daraja jipya la Selander, kuanzia kesho Februari 1, 2022, baada ya kukamilika kwa asilimia 100.
Amesema kwamba, daraja hilo litaruhusiwa kwa wananchi kulitumia bila malipo kwa saa 24 kwa siku.
Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kukagua daraja hilo.
Amesema “Daraja hili ni muhimu sana kwa sababu litapunguza changamoto ya foleni, daraja la zamani la Selender lilikuwa limezidiwa na wingi wa magari, hivyo kukamilika kwake ni mwarobaini kwa foleni za jiji la Dar es Salaam”,
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kutoa fedha za ujenzi na matengenezo ya miundombinu nchini ili Tanzania kufunguka zaidi katika miundombinu, hivyo kuchochea uchumi wa Taifa.
Akizungumzia barabara ya Jangwani, Profesa Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hiyo, haukuzingatia mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali itaanza kujenga daraja jipya ambalo litaruhusu maji kupita pia eneo la Kariakoo ambako miundombinu yake tutaiboresha,’’amesema.
Pia, amewataka mameneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kila mkoa, kuhakikisha madaraja yote nchini, yanazibuliwa ili maji yapite bila kikwazo.
Amesema kuwa, hatua hiyo itasaidia miundombinu kuwa salama na kuepusha uharibifu nyakati za mvua, itakayoepusha ujenzi wa mara kwa mara.
Kwa upande wa daraja la Selander Profesa Mbarawa alisema, ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 huku akieleza kuwa ni muhimu kwa kuwa utapunguza muda mwingi unaotumiwa na wananchi kuingia na kutoka mjini.
“Tunaamini kupitia daraja hili watu watafanya majukumu yao vyema, awali watu walikuwa wakitumia saa moja ila sasa watatumia dakika 30 pekee,’’alisema.
Profesa Mbarawa alielekeza TANROADS katika kudhibiti ajali, waweke alama za barabarani kwa kuwa kumekuwa na ajali nyingi katika baadhi ya maeneo na nyingi zikisababishwa na uzembe wa madereva na barabara zenyewe.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila, alisema ujenzi wa daraja jipya la Selander umekamilika kwa asilimia 100 na kinachoendelea sasa ni uwekaji wa vifaa vya usalama.
Mhandisi Mativila alieleza daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03 hadi kukamilika kwake serikali imetumia sh.bilioni 243 na litazinduliwa Februari Mosi, mwaka huu.
WANANCHI WANENA
Akizungumzia hatua hiyo, dereva teksi Athuman Bakari amesema kuanza kutumika kwa njia hiyo kutawarahisishia wananchi kutokaa muda mrefu katika foleni.
Pia, alisema daraja hiyo litawasaidia kupunguza gharama mafuta kwa kuwa watakuwa wakitumia muda mfupi kwenda na kurudi mjini.
Naye, dereva teksi Aboubakar Swahib, alisema daraja hilo ni mkombozi mkubwa kwao na wakazi wa maeneo hayo kwa kuwa litawarahisishia kwenda na kurudi nyumbani au kazini.
Mkazi wa Masaki, Dar es Salaam, Dk. Zanifa Omary alisema kwa kawaida asubuhi barabara ya Ali Hassan Mwinyi huwa na foleni, hivyo kuanza kutumika kwa daraja la Tanzanite litawaondolea wananchi changamoto ya kukaa muda mrefu barabarani.
“Asubuhi huwa kuna foleni katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, hivyo kuanza kutumika kwa daraja la Tanzanite litapunguza foleni na njia itakuwa fupi kwa kuwa magari yatakayopita katika daraja hilo yatatokea hospitali ya Aga Khan,” alisema na kuwasihi wananchi kulitumia kwa uangalifu ili lidumu kwa muda mrefu.
Diwani wa Kata ya Kivukoni, Sharik Choughle, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa daraja, kwa kuwa foleni mara nyingi husababisha kuzorota kwa kazi, hivyo uwepo wa madaraja hilo utarahisisha shughuli za maendeleo kwenda kwa kasi.
Na BARAKA LOSHILAA