Na THABIT MADAI, ZANZIBAR
MKURUGENZI Mtendaji Tume ya Kitaifa ya Uratibu na Udhibiti wa dawa za kulevya Zanzibar, Luteni Kanal Burhani Zuberi Nassor, amesema dawa za kulevya zimekuwa tishio Zanzibar huku akiitaka jamii ishirikiane katika malezi ya vijana, ili kuepusha balaa kubwa zaidi.
Ametoa kauli hiyo leo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya dawa za kulevya, yanayotarajiwa kufanyika Juni 26, mwaka huu na kuhudhuriwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Burhan amesema dawa za kulevya hivi sasa ni tishio Zanzibar na kwamba vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa, wamekuwa waathirika wakubwa wa dawa hizo.
“Tuwe na mashirikiano kwa kuwa karibu na watoto na iwapo unamuona na kitu ambacho kiko nje ya uwezo wake, kifatiliwe ili kumnusuru na janga hilo kwani tusipokuwa imara wazazi basi baada ya miaka 20 kila nyumba itakuwa na mteja.
“Jamii tuondoe huruma kwa kulindana mitaani bali tutoe taarifa kwa vyombo vinavyohusika kwa kila anayefanya biashara hiyo ili kupunguza kadhia hii ambayo imekuwa kila sehemu katika mitaa yetu.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti na Uchukuzi Juma Zidikheiry, amesema ripoti za kitengo cha Polisi cha kupambana na dawa za kulevya zimeonesha katika kipindi cha miaka 9 iliyopita, kuanzia 2012, umla ya watuhumiwa 3,810 wakiwemo wanaume 3,577 na wanawake 233 wamekamatwa nchini wakijihusisha na uhalifu wa dawa za kulevya .
Hata hivyo, amesema katika kipindi hicho jumla ya kilo 51.5 za heroini kilo 2,946 za bangi, kilo 5.4 za valiamu na kilo 19.71 za kokeni zilikamatwa.