MKUU wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Jokate Mwegelo, amesema wanatarajia kujenga shule za sekondari katika kata ambazo hazijajengewa shule hizo.
Pia, amesema watajenga fensi katika shule zote wilayani humo, ili kuepusha utoro na kuimarisha usalama kwa wanafunzi.
Jokate aliyasema hayo jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ujenzi huo utaanza hivi karibuni kwa kutumia fedha za mapato ya ndani za halmashauri.
“Fedha tunazo za kutosha kwa kuwa sisi tunaongoza kwa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zote nchini. Hivyo tutatekeleza suala hili kwa haraka ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa na shule za sekondari kila kata,” alisisitiza.
Jokate alisema mkurugenzi wa manispaaa hiyo na wataalamu wake wameshaanza kuyaandaa maeneo ya ujenzi huo.
Kuhusu ujenzi wa fensi za shule, mkuu huyo wa Wilaya alisema mwaka huu wa fedha wameweka bajeti ya kutekeleza hilo.
“Kukosekana fensi katika shule ni moja ya chanzo cha utoro kwa wanafunzi, tutatekeleza haraka katika shule za msingi na sekondari,” alisisitiza.
Jokate alisema wanashirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri Temeke, Elihuruma Mabelya, watumishi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutatua kero za wananchi hao.
“Tutahakikisha tunatekeleza maagizo yote ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wakati na weledi, katika majukumu ambayo ameamini tunaweza kumsaidia,” alisisitiza.
Mabelya alisema watakamilisha ujenzi wa maabara kwa shule ambazo hazijakamilisha na zile ambazo hazijapata.
“Zipo shule zenye maabara moja, zingine mbili na zingine hazina kabisa, hivyo katika mwaka huu wa fedha tutazikamilisha na kuweka vifaa vyake ili kuondoa changamoto hiyo kwa wanafunzi,” alisema.
Pia, aliahidi watatatua changamoto za maji katika shule ambazo hazina huduma hiyo au kuwepo kwa kiwango kisichotosha.
“Baadhi ya shule zina matenki ya maji madogo yasiyotosheleza, tutahakikisha tunawapa vifaa vikubwa zaidi,” aliahidi.
Mkurugenzi huyo alimpongeza Rais Samia kuwapa fedha za uboreshaji wa miundombinu ya elimu, huku akiahidi watahakikisha wanasimamia vyema taaluma ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
Na SUPERIUS ERNEST