WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara DK. Ashatu Kijaji, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya kazi kubwa ya kuimarisha diplomasia ya uchumi na mataifa mengine jambo ambalo lililoimarisha uwekezaji na biashara nchini.
Amesema hatua ya Rais Samia kufanya ziara nje ya nchi ikiwemo Dubai, Ufaransa, Burundi, Kenya na Ubelgiji imewezesha kufungua milango ya kibiashara na kupanua wigo wa fursa za uwezekezaji nchini hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi.
Akizungumza Dar es Salaam, Waziri Dk. Kijaji amesema ziara hizo za kuhimarisha Diplomasia ya uchumi baina ya Tanzania na mataifa mengine, zimefanikiwa.
Alibainisha kuwa katika mwaka mmoja wa mafanikio wa Rais Samia, jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya sh. trioni 18.75 imesajiliwa nchini ambayo itatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 62,301.
“Nchi yetu imeingia katika historia mwaka mmoja wa Rais Samia, umeleta neema kwa Watanzania kwa kuwa imefungua milango ya diplomasia na uchumi hali iliyosababisha kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya sh. trioni 18.75,” alisema.
Dk. Kijaji alisema miradi hiyo itatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 62,301 kiwango ambacho hakikuwahi kutokea katika uandikishwaji na usajili wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) tangu taifa kupata uhuru,”alisema.
Alisema mbali na mafanikio hayo, makubwa waliyoyafikia sasa, bado wanatarajia matokeo zaidi kutokana na ziara hizo katika makongamano ya kimataifa.
Akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya Dubai 2022 yamekuwa ya mafanikio kwa serikali na sekta binafsi kwa kuwa yametoa fursa za kutangaza biashara na uwekezaji.
“Rais Samia alihudhuria maonesho hayo siku ya kifaifa yaliyoudhuliwa na mataifa 192 na wafanyabiashara 500 ambapo 200 walitoka Tanzania na 300 kutoka mataifa mengine,” alisema.
Dk. Kijaji alisema maeneo hayo yalikuwa ya manufaa kwa Tanzania kwa kuwa iliingia hati za makubaliano 37 zilizosainiwa kati ya Tanzania na mataifa mengine.
Waziri Dk. Kijaji alisema hati hizo zinathamani ya dola bilioni nane sawa na sh. trilioni 18.5 za Kitanzania. Pia alisema hati hizo zinatarajiwa kutoa ajira 214,475.
“Kutekelezwa kwa miradi hii mikubwa kama ambavyo Rais Samia anaagiza itekelezwe kwa kasi mafanikio makubwa yatapatikana ambapo ni jambo la kujivunia kupata fedha hizo nyingi ndani ya mwaka mmoja,” alisema
Alieleza kuwa katika hati hizo 37 zilizosainiwa 14 zilikuwa ni baina ya serikali na wizara zake na zile za kutoka mataifa mengine, 23 zilisainiwa baina ya taasisi binafsi za nchini na mataifa mengine huku hati moja ikisainiwa baina ya Zanzibar na taifa lingine.
Alisema kusainiwa kwa hati hizo za sekta binafsi ni dhamira ya dhati ya Rais Samia kuendeleza sekta hiyo muhimu nchini ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia pato la taifa.
Dk. Kijaji alisema mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia ni kurahisisha upatikanaji wa vibali vya wageni kwa kubadilisha baadhi ya sheria.
“Kwa sasa sheria inaruhusu wawekezaji kuleta wataaalamu 10 kutoka nje ya nchi, tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo waliruhusiwa wataalamu watano tutoka nje ya nchi jambo ambalo linasaidia pia kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kutoka kwa wageni hao,” alisema.
Waziri Kijaji alisema Serikali imeunganisha mifumo ya kielektroniki ili kuraisisha utoaji wa vibali kwa wageni ambayo itaunganisha na maombi ya mtandao ya vibali vya wakazi hali itakayowaondolea usumbufu wa kupata vibali wawekezaji wanaokuja nchini.
NA SUPERIUS ERNEST