NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameagiza maombi 521 ya umilikishaji ardhi Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kukamilishwa ndani ya siku tatu.
Dk. Angeline alitoa agizo hilo alipofanya ziara katika ofisi ya ardhi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto, anachotaka maombi 521 yawe yamekamilika katika kipindi cha siku tatu.
“Kuanzia sasa, tunahitaji zile ‘applications’ zote ambazo hati zake watu wameomba, zitoke ndani ya siku tatu kama ni kutoka saa 8.00 usiku, tunahitaji hiyo kazi ikamilike ndani ya siku tatu,’’ alisema.
Aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika jiji la Dodoma, kuandaa hati zisizopungua mia moja kwa siku moja pamoja na kuwataka kumhakikishia kwa maandishi, ahadi walizompa kutekeleza maagizo hayo.
Uamuzi wa Dk. Angeline wa kufanya ziara ya kushtukiza ofisi ya ardhi katika jiji la Dodoma, unatokana na baadhi ya malalamiko ya ucheleweshaji umilikishaji ardhi kwa wananchi wa mkoa huo, jambo lililofanya wizara kuanza mkakati maalumu wa ukwamuaji na uharakishaji wa suala hilo.

Awali, Naibu Waziri huyo na timu yake, walitembelea vitengo vya ardhi katika halmashauri ya jiji la Dodoma ili kubaini baadhi ya changamoto.
Kwa mujibu wa Dk. Angeline, jiji la Dodoma ndiyo sura ya nchi, hivyo maofisa wake wa ardhi wanatakiwa kuwapanga wananchi wanaokwenda kupata huduma kulingana na maeneo wanayotoka pamoja na maofisa hao, kuvaa vitambulisho ili kutambulika na wananchi.
“Hatuhitaji kusikia kelele za watu hapa, ninyi mnachafua image (Taswira) ya Wizara na sekta kwa sababu tu ya kutojipanga katika utendaji wenu wa kazi.
“Mko wengi mnaweza kujipanga vizuri na kuwepo upungufu wa watumishi kwa baadhi ya maeneo,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mary Makondo, alisema kuwa, wamejipanga kuhakikisha kasi inaongezeka ya umilikishaji ardhi katika mkoa wa Dodoma na maeneo mengine nchini.
Katika jitihada za ukwamuaji na kuongeza kasi ya utoaji hati katika jiji la Dodoma, Wizara yake imeamua kuongeza nguvu ya watumishi kutoka Makao Makuu ili kuharakisha zoezi hilo liweze kukamilika kwa wakati.
Naye, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Halmashauri ya jiji la Dodoma, Amelyo Chaula, aliweka wazi kuwa, mwamko mkubwa umilikishaji ardhi kutoka kwa wananchi umesababisha ofisi yake kuelemewa na kazi.
Hata hivyo, alisema ofisi hiyo imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati pamoja na kuwepo changamoto kadhaa kwa baadhi ya maeneo hasa yale yaliyorithiwa kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kusisitiza kuwa, maeneo mapya hayana changamoto ya Umilikishaji.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma