WAZIRI wa Madini, Dk. Doto Biteko, amewaagiza mkuu wa wilaya ya Bunda, ofisa madini mkazi na katibu tawala wa mkoa kuhakikisha wanafungua Soko la Madini wilayani Bunda, ili kuwarahisishia wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kupata huduma hiyo karibu.
Agizo hilo alilitoa Desemba 28, 2021, alipokuwa akizungumza na wachimbaji katika eneo la Kinyambwiga, lililoko Kata ya Guta, wilayani Bunda, mkoani Mara.
“Natoa agizo kwa mkuu wa wilaya, ofisa madini na katibu tawala wa mkoa ambaye kwa mujibu wa kanuni ya uanzishwaji wa masoko ya madini ndiye mwenye kutafuta eneo sahihi ya kuweka soko la madini.”
“Haiwezekeni mchimbaji ana dhahabu yake mfukoni halafu anakeenda hadi Musoma kutafuta soko,”alisema.
Dk. Biteko alisema ni lazima soko la madini lianzishwe Bunda ili watu wafanye biashara kwa urahisi.
Alisema kuna umbali mkubwa kutoka eneo la machimbo mpaka Bunda na kuwataka waanzishe kituo kidogo cha kununua madini katika eneo la Kinyambwiga.
Waziri huyo alisema eneo liandaliwe kwa wafanyabiashara wa madini ili biashara ifanyike.
Na Mwandishi Wetu