WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Dk. Selemani Jafo, amewahimiza wananchi kutumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kupanda miti ili kufikia lengo lililowekwa la kupanda miti Milioni 276 nchi nzima.
Aidha, ili kufikia malengo hayo amewaasa pia wanafunzi kuendeleza kampeni ya Soma na Mti aliyoizindua hivi karibuni yenye lengo la kupanda miti zaidi ya Milioni 14.
Waziri Dk. Jafo, ametoa maagizo hayo jijini Dodoma katika zoezi la upandaji miti katika eneo la Medeli ikiwa ni sehemu ya shughuli iliyoanza kutekelezwa katika wiki ya uzinduzi wa Sera ya Mpya ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 ambayo inatarajiwa kuzinduliwa Februari 12 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Dk. Jafo amewakumbusha wadau wote kushirikiana katika kuibeba ajenda ya upandaji na utunzaji wa miti ili kuondokana na changamoto ambazo zilianza kujitokeza ikiwemo ukosefu wa mvua uliopelekea mabwawa kukauka na kusababisha uwepo wa mgao wa umeme.
“Niziombe familia tumesema tuna lile jukumu la kupanda miti ili kuitendea haki Tanzania yetu, tufanyie kazi ajenda ya mazingira sababu maji yalipungua kwenye vyanzo vingi vya mabwawa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi,”amesema.
Shughuli nyingine zitakazotekelezwa katika wiki hiyo ni upandaji wa miti katika eneo la Iyumbu, Isern, maeneo ya barabara inayoanzia Chimwaga na Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam.
Aidha, usafi utafanyika pembezoni mwa barabara inayoanzia Shule ya Martine Luther hadi wajenzi kupitia Nzughuni, Ilazo, Ipagala na Area C, kutoa elimu kuhusu utenganishaji wa taka, kufanya usafi katika soko la Chang’ombe na utoaji wa elimu ya mazingira kwa wananchi na wadau kupitia vyombo vya habari.
NA SELINA MATHEW, DODOMA