KAMISHNA Jenerali wa Uhamaji Nchini, Dk. Anna Makalala, amesema vyombo vya ulinzi na usalama vipo macho na vitamkamata yeyote atakayethubutu kuhifadhi au kusafirisha wahamiaji haramu.
Alisema hayo mkoani Kigoma wakati wa ziara yake na kwamba, Uhamiaji iko makini.
Pia, Dk. Makalala aliwaonya watu wanaofanya biashara hiyo, kuacha mara mmoja vinginevyo watakumbana na mkondo wa sheria.
“Hapa Kigoma, nawaomba mdumishe amani, naomba muache kabisa vitendo vya kusafirisha na kuhifadhi wahamiaji haramu, vitendo hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria ya Uhamiaji sura 54 Rejeo la mwaka 2016 pamoja na kanuni zake,”alisema.
Dk. Makalala alisema watu watakaokamatwa na kuthibitika kutenda makosa hayo, adhabu ni kifungo cha miaka 20 au kulipa faini isiyopungua sh. milioni 20 au vyote kwa pamoja.
Alisema ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu nchini uhamiaji inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, mitandao ya kijamii na machapisho ili kujenga uelewa kwa wananchi juu ya athari za kuwakumbatia wahamiaji hao.
Dk. Makalala aliwataka wananchi wa Kibirizi kutoa ushirikiano katika suala la ulinzi na usalama, kwani jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la kila mwananchi.
Kamishna Jenerali huyo, alitoa elimu ya uraia kwa wananchi wa mkoa huo na kueleza kwamba, hakuna raia wa daraja A wala B , wote ni sawa na wanapata haki katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa kiutamaduni na kijamii.
Katika ziara hiyo, Dk. Makalala alifanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa na maofisa, askari, watumishi na askari wa Uhamiaji.
Akizungumza na askari huyo, Kamishna Jenerali huyo aliwataka maofisa, askari na watumishi raia kudumisha nidhamu, utii, uhodari na kufanya kazi kidiplomasia na kwa weledi wa hali ya juu ili Kukuza uchumi wa taifa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Dk. Makalala aliwataka askari hao, kusimamia vyema ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanayotokana na huduma mbalimbali za kiuhamiaji.
Ziara ya kamishna Jenerali Dk. Anna Makalala ni mwendelezo wa ziara zake anazozifanya nchi nzima.
Na MWANDISHI WETU, Kigoma