MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kuongeza kasi ya utafiti na kuzalisha dawa bora za asili.
Dk. Mpango alitoa agizo hilo, wakati akifungua Mkutano wa 31 wa pamoja wa Sayansi ulioandaliwa na taasisi hiyo ambao uliofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo, unawashirikisha wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kutoka maeneo ya ndani na nje.
Aliiagiza taasisi hiyo kuongeza kasi ya ufanyaji utafiti na kuzalisha chanjo na dawa bora za asili.
Makamu wa Rais, alisema Serikali imedhamiria kufikisha huduma za kiafya katika maeneo yote nchini na itaendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo watafiti na sekta binafsi.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, Tanzania inaunga mkono na kuamini katika ufanyaji wa tafiti zitakazokabiliana na changamoto za maradhi nchini.
Alisema mkutano huo ni fursa ya aina yake kwa wanasayansi wa Tanzania, kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuunganisha werevu na uwezo katika kupata suluhisho la kimsingi kwa changamoto kuu za kiafya nchini.
Makamu wa Rais alisema mkutano huo una umuhimu mkubwa kutokana na kufanyika katika kipindi ambacho dunia, Tanzania ikiwemo, inapitia katika changamoto mbalimbali za magonjwa ukiwemo ule wa Uviko 19 na magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi hiyo ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.
Alisema tayari NIMR imeshiriki katika tafiti mbalimbali zinazowezesha utungaji sera na mipango katika wizara hiyo kama kuwezesha kupata uhalisia wa utoaji chanjo ya HPV ambayo inakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
Na MWANDISHI WETU