Na REHEMA MAIGALA
MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, amewataka viongozi wa dini kufuata mwenendo wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, katika utumishi wa miaka 50 wa daraja la Upadre.
Amesema Kardinali Pengo, amekuwa nguzo muhimu ya kuunganisha serikali, kukemea maovu na kuleta amani na mshikamano katika taifa.
Akizungumza jana katika hafla ya Misa Takatifu ya Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya utumishi wa Mwadhama Polycarp Pengo, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria, Msimbazi Dar es Salaam, Dk. Mpango alisema siku zote wakristu wanatakiwa kuyakumbuka mazuri aliyofanya Kardinali Pengo.
Dk. Mpango alisema Kardinali Pengo, ameacha mazuri mengi ndani ya serikali hasa katika kipindi chake cha Utume ndani ya Jimbo la Dar es Salaam ukiwemo unyenyekevu na usuluhishi.
Alisema siyo viongozi wa dini pekee wanaotakiwa kuiga mfano wake mzuri aliouonyesha ndani ya Kanisa Katoliki, bali hata viongozi wa serikali wanatakiwa kufuata nyayo hizo.
Hata hivyo, Dk. Mpango alimwomba Kardinali Pengo aendelee kuwaombea viongozi wa mamlaka zote ili wawe na roho ya hekima katika majukumu yao kila siku.
“Tunakutegemea katika sala zako baba, usichoke kuliombea taifa lako na viongozi waliopo ndani yake, ili waendelee kuwa na roho za hekima katika majukumu yao mbalimbali,” alisema.
Dk. Mpango alimsifu Cardinal Pengo kwa kutimiza miaka 50 ya daraja la upadre ambalo amepitia katika mambo mengi ikiwemo dhoruba na furaha.
SALAMU ZA RAIS SAMIA
Akitoa salamu za Rais Samia Suluhu Hassan, Dk. Mpango alisema Rais anamwomba Kardinali Pengo kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali na wananchi ili amani na utulivu iendelee daima.
Dk. Mpango alisema serikali ya awamu ya sita, inaahidi kuendeleza miradi yote ya kimaendeleo aliyoiacha Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli.
Katika ibada hiyo Dk. Mpango alitoa zawadi kwa niaba ya serilkali ambazo ni cheti cha shukrani cha kutambua uongozi wake uliotambuka ndani ya kanisa la Kikatoliki kiichotolewa na Rais Samia.
Pia, ilitoa fedha kwa ajili ya mwendelezo wa ujenzi wa Kanisa la Makulunza lililopo Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
“Pokea zawadi hizi kutoka serikalini kwa kutambua mchango wako mkubwa uliouonesha ndani ya Kanisa,” alisema.
KARDINALI PENGO
Akizungumza katika hafla hiyo, Cardinal Pengo alisema amekuwa Askofu Mkuu katika awamu zote za serikali kuanzia ile ya Hayati Mwalimu Julias Nyerere na amekuwa na mahusiano ya baraka na serikali katika kipindi chote cha uaskofu.
“Nimekuwa Askofu kwa kipindi kirefu kuanzi enzi ya Mwalimu Nyerere hadi leo hii nipo naendelea kuiombea nchi yangu ya Tanzania katika mema yote,” alisema.
Kadhalika Kardinali Pengo alimuomba Dk. Mpango afikishe shukrani zake kwa Rais Samia pamoja na viongozi wengine wote.
Pia, alimshukuru Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi kwa kupokea dhamana hiyo ya uaskofu.
“Namshukuru Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kwa kuendelea na uaskofu katika jimbo hili kipindi ambacho mimi afya yangu ilikuwa si nzuri,” alisema
RAIS WA BARAZA LA MAASKOFU
Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Gervas Nyaisonga alimpongeza Kadrinali Pengo kwa utume wake ambao haujawahi kutetereka wakati wa dhoruba na furaha.
Alisema utume wa Kardinali Pengo umeweza kuzaa matunda mema ndani ya kanisa la kikatoliki.
Alisema Kardinali Pengo alipokea Jimbo la Dar es Salaam kukiwa na Parokia 20 lakini hadi anastaafu ameacha parokia 126.
“Ni jambo la pongezi na kumshukuru Mungu kwa kumpata kiongozi ambaye alikuwa mahili ndani ya kanisa la Kikatoliki”,alisema.
“Tunatakiwa tumuenzi Pengo kwa kuzingatia yale aliyotufundisha siku zote, na kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Cardinal Pengo alipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa viongozi wa serikali na dini walioudhuria misa hiyo takatifu.