MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amemtaja Dk. Mwele Ntuli Malecela, kuwa ni shujaa aliyejitoa kupigania afya za wananchi kupitia tafiti alizozifanya zenye lengo la kusaidia jamii kupambana na magonjwa mbalimbali.
Dk. Mpango aliyasema hayo alipokwenda kumpa pole Waziri Mkuu mstaafu, Samwel Malecela, nyumbani kwake Mtaa wa Kilimani, jijini Dodoma, kutokana na kifo cha mtoto wake, Dk. Mwele, kilichotokea Februari 10, mwaka huu, Geneva, nchini Uswisi.
Amesema Dk. Mwele alifanya kazi iliyo njema na kuonekana katika jamii ndani na nje ya nchi.
Makamu wa Rais alisema Dk. Mwele katika kipindi cha uhai wake, aliinua jina la Tanzania kwa kuaminiwa kufanya kazi katika taasisi kubwa ya afya duniani.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, uwezo wa Dk. Mwele katika kazi uliinua wanawake nchini, hivyo hakuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hiyo na kumuombea ampokee ili apumzike kwa amani.
Aliwasihi waombolezaji kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu na kumuombea marehemu apate pumziko la amani.
