MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kutoa uamuzi wa mwisho wa uwekezaji mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, nchini Uganda hadi Chongoleani nchini Tanzania (EACOP).
Hafla hiyo imefanyika katika uwanja wa sherehe wa Kololo, ulioko Kampala, nchini Uganda na kuhudhuriwa na kampuni mbalimbali za kimataifa ambazo ni wabia wa mradi huo.
Taarifa iliyotolewa mapema asubuhi na Msaidizi wa Makamu wa Rais (Habari), Franco Singaile, ilieleza kuwa, Dk. Mpango aliondoka nchini kwenda Kampala nchini Uganda ambako alishiriki katika hafla hiyo.
Ilisema Dk. Mpango alikwenda Kampala, kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
“Akiwa nchini Uganda, Dk. Mpango atamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kutoa uamuzi wa mwisho wa uwekezaji katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanzania (EACOP),” ilisema.