MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, ametoa maagizo tisa kwa Wizara ya Madini, wawekezaji na wadau wengine katika sekta hiyo, akitaka yafanyiwe kazi kwa ustawi na kuimarika zaidi kwa sekta ya madini nchini.
Miongoni mwa maagizo hayo ni wawekezaji katika miradi ya ubia na serikali kuharakisha utekelezaji, wachimbaji kuzingatia sheria za usimamizi wa mazingira na wawekezaji kutojihusisha na ajira za watoto akiwataka wawekeze kutoa utaalamu kwa jamii.
Dk. Mpango ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini, uliobeba kaulimbiu isemayo, ‘mazingira wezeshi kwa maendeleo ya sekta ya madini’.
Amewataka wawekezaji katika miradi ya ubia na serikali kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ili Watanzania waanze kunufaika na fursa zitakazotokana na uwekezaji husika.
Dk. Mpango amewasisitiza wachimbaji wote kuzingatia sheria za usimamizi wa mazingira kwa kuwa uchimbaji wa madini unaenda sambamba na uharibifu wa mazingira.
“Aidha wawekezaji wote mnao wajibu wa kuhakikisha shughuli zenu za uchimbaji, uchenjuaji na uchakataji wa madini zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria na taratibu ili tunufaike kikamilifu na rasilimali zetu sambamba na ninyi kupata faida,” alisema.
Agizo la tatu aliwataka wawekezaji wote hasa wakubwa kuzingatia matakwa yanayotokana na tathmini ya athari kwa mazingira na jamii.
Aliongeza pia wazingatie misingi ya uzalishaji endelevu, matumizi ya mbinu bora za uzalishaji na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.
Katika agizo lake la nne, Dk. Mpango aliwaasa wawekezaji na wachimbaji kutojihusisha na ajira za watoto, badala yake waongeze juhudi hasa katika kuhamasisha, kujenga uelewa na kukuza uwezo wa jamii na wachimbaji wadogo hususan wanawake, kupitia wataalamu wao na teknolojia.
Aliziagiza kampuni zinazowekeza katika sekta ya madini kuhakikisha zinatekeleza ipasavyo takwa la kisheria la kuandaa mipango ya ufungaji migodi na kuweka hati fungani ya urekebishaji wa mazingira.
Agizo la sita, alilitoa kwa benki na taasisi nyingine za fedha kwa kushirikiana na Shirika la Madini (STAMICO), kubudi namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wakati serikali inafanyia kazi suala la kuanzisha benki maalumu ya madini.
Aliwahimiza wawekezaji wakubwa kuendelea kuboresha uchumi wa wananchi katika maeneo yenye migodi kwa kutoa fursa za ajira katika migodi yao na kujenga urafiki na jamii zinazowazunguka ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Hata hivyo, alimuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kupeleka taarifa ya halmashauri zinazowatoza wachimbaji tozo zisizofahamika na Wizara ya Fedha na Mipango, ili zishughulikiwe.
Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko, alisema katika mkutano wa mwaka jana, walitoka na maazimio mbalimbali na hata mkutano huu yote yaliyosemwa wanayachukua na kwenda kuyafanyia kazi.
Alieleza sekta hiyo imeendelea kukua na wawekezaji wameongeza imani ya kuwekeza katika madini, kutokana na maboresho ya kisera na sheria yaliyofanywa na serikali.
Alisema kumekuwa na wawekezaji wengi waliojitokeza katika kujenga mshine za kusafisha dhahabu na changamoto ni upatikanaji wa dhahabu ya kutosheleza mashine hizo.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, alisema kundi hilo hukabiliwa na changamoto ya kukosa mitaji ya kuendeshea shughuli zao.
Mkutano huo pamoja na viongozi wa Tanzania, Mawaziri na Naibu Mawaziri wa nchi za Burundi, Zimbabwe, Comoro, Sudan Kusini, Sudan na Libya na Mabalozi wa nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walihudhuria.
NA JUMA ISSIHAKA