MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Watanzania waishio Singapore kwa kuwahakikishia kwamba, serikali inatambua na kuthamini mchango wao.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais aliwaeleza Watanzania hao wanaoishi nje ya Tanzania kwamba, serikali inatambua mchango wao katika ujenzi wa taifa na hivyo, itaendelea kutatua changamoto zote zinazokwamisha wao kuwekeza nchini.
Makamu wa Rais alisema kuanzishwa kwa Idara Maalum inayoshughulikia Masuala ya Watanzania wanaoishi Nje ya Tanzania katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ni ishara thabiti ya kutambua kwa vitendo mchango wa diaspora katika taifa.
Dk. Mpango aliwakaribisha Watanzania hao kuwekeza nchini huku akiwakikishia kwamba, serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo katika kuvutia uwekezaji pamoja na kuboresha sekta ya biashara.
“Serikali itaendelea kupokea maoni na ushauri kutoka kwa diaspora katika yale ambayo yataleta mchango wa ujenzi wa Tanzania,” aliongeza.
Makamu wa Rais alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeendela kuimarisha uhusiano wa kimataifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 na kuongeza, Rais amedhamiria kuendeleza miradi yote mikubwa ilioanzishwa katika awamu ya tano na kuendelea kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali za Watanzania katika sekta mbalimbali, zikiwemo za afya na elimu.

DIASPORA
Kwa Upande wao Watanzania hao wanaoishi nchini Singapore wamepongeza jitihada zinazochukuliwa na Tanzania katika kutafuta muafaka wa hadhi maalum kwa ajili yao, ili kuwapa nafasi ya kuwekeza kikamilifu nchini.
Waliiomba serikali kuendelea kutatua changamoto hasa katika masuala ya kodi pamoja na vibali vya kazi kwa wataalam mbalimbali wanaolenga kuwaleta kutoa huduma Tanzania.
NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, alisema wizara inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kutafuta muafaka wa kuwapa hadhi maalum diaspora na kuwakaribisha kurejesha ujuzi walioupata nchi za nje katika kujenga uchumi wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Heshima wa Tanzania Nchini Singapore, Teo Sieng Seng, mazungumzo yaliofanyika katika Hoteli ya Raffles, nchini humo.
Makamu wa Rais alimpongeza balozi huyo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuitangaza Tanzania huku akimueleza kwamba, nchi ni salama na yenye utulivu na amani hali inayovutia wawekezaji hivyo, kumuomba kuendelea kutoa mchango wake katika kukuza biashara, kuongeza watalii na wawekezaji.
Na Mwandishi Wetu