MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, amewashukuru Watanzania kwa kumpa faraja baada ya msiba wa kaka yake, Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Gerald Mpango, kilichotokea Januari mwaka huu.
Dk. Mpango alitoa shukrani hizo wakati akishiriki Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya tatu ya mwaka C wa Kanisa katika Kanisa Kuu Katoliki la Bikira Maria Mshindaji Jimbo la Kigoma.
Aliwashukuru waumini wa kanisa hilo, wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla waliompa faraja na familia kutokana na kifo cha kaka yake.
Dk. Mpango aliyeongozana na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango, katika ibada hiyo, aliwasihi waumini wa kanisa hilo, kuliombea taifa na viongozi wake.
Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo la Kigoma, Joseph Roman Mlola, Dk. Mpango alisisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani na utulivu ili kumtukuza Mungu katika mazingira salama.
Hata hivyo, aliwapongeza waumini wa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mshindaji Jimbo la Kigoma kwa kujitoa katika kukamilisha ujenzi wa kanisa.
Katika hatua nyingine, Dk. Mpango aliendesha harambee kwa wasaidizi wake waliokuwepo kanisani hapo na kukusanya sh. milioni 1.3 na kuzikabidhi kwa ajili ya maendeleo ya kanisa hilo.
NA MWANDISHI WETU