Na MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amependekezwa na kuthibitishwa kwa kishindo bungeni kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Pia, Makamu huyo wa Rais Mteule ataapishwa kesho Ikulu, Chamwino jijini Dodoma, mbele ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, kushika wadhifa huo, atakaoutumikia kwa kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo inakuja baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais kuapishwa kuwa Rais, kufuatia kifo cha Hayati Dk. John Magufuli.
Jina la Dk. Mpango limewasilishwa Bungeni jijini Dodoma leo na Mpambe wa Rais baada ya Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichofanyika jijini humo.
Baada ya jina hilo kuwasilishwa bungeni Wabunge 363 ikiwa ni idadi ya wabunge wote nchini, walipiga kura za ndiyo na kumfanya Dk. Mpango kuthibitishwa kwa asilimia 100 katika nafasi hiyo.
Dk. Mpango anaukwaa wadhifa huo, kutoka kuwa Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma.