MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango anatarajiwa kuzindua Sera mpya ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 yenye maeneo mapya sita Februari 12 mwaka huu jijini Dodoma.
Sera hiyo imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwemo katika sera ya mwaka 1977 na mapya ikiwa ni pamoja na udhibiti wa taka za kielektroniki, uchafuzi katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, usimamizi wa matumizi ya kemikali, mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti viumbe hai na usimamizi wa matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mary Maganga, amesema hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa mchakato wa mapitio wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997.
Amebainisha kuwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imeongeza wigo wa masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu.
Vilevile, Sera mpya imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani.
“Kama nilivyoeleza awali kuhusu uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 Serikali imeamua kuwa na Wiki ya Uzinduzi wa Sera itakayoanza Februari 7 hadi 12 ambapo shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira zitafanyika ikiwa ni sehemu ya masuala ya msingi yanayoelekezwa katika Sera mpya,”amesema.
Ameeleza dhumunii la kuwepo kwa shughuli hizo ni pamoja na kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kwa kuwa na zoezi la upandaji miti.
“Ili kuwa na mazingira safi, kutakuwa na shughuli za usafi wa mazingira zinazolenga kuboresha afya ya jamii na elimu ya utenganishaji taka kwa ajili ya udhibiti wa taka ngumu na kuwezesha urejelezaji wa taka kwenye bidhaa na huduma mbalimbali,”amesema.
Amefafanua kuwa, shughuli zitakazotekelezwa katika Wiki ya Uzinduzi ni pamoja na upandaji miti jijini Dodoma katika maeneo ya Medeli Februari 7, Iyumbu Februari 8, Isern Februari 9, maeneo ya barabarra inayoanzia Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam Februari 12.
Aidha, kufanya usafi pembezoni mwa barabara inayoanzia Shule ya Martin Luther hadi Wajenzi kupitia Nzuguni, Ilazo, Ipagala na Area C, kutoa elimu kuhusu utenganishaji wa taka na kufanya Usafi katika soko la Changombe na utoaji wa Elimu ya Mazingira kwa wananchi na wadau kupita vyombo vya habari ambapo zote zitaanza saa 1:00.
“Ninapenda kuwaalika wadau wote wa mazingira nchini hususan wa Mkoa wa Dodoma na viunga vyake kushiriki katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira pamoja na shughuli zote zitakazofanyika katika Wiki ya Uzinduzi wa Sera,”amesema.
NA SELINA MATHEW, DODOMA