RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), una mchango mkubwa katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Zanzibar, alipokutana kwa mazungumzo na uongozi wa juu wa UWT, uliofika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza sambamba na kumtambulisha Katibu Mkuu mpya wa Umoja huo, Phillis Nyimbi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema UWT umekuwa ukishiriki vyema katika kuhakikisha CCM, kinaendelea kushika hatamu na kuimarika kwa lengo la kuiletea maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake.
Alisema umoja huo, umekuwa nguzo muhimu katika kukiimarisha Chama na umeweza kusaidia katika harakati zote, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha CCM kinaendelea kushika madaraka katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka jana 2020, ambao CCM kilishinda kwa kishindo.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuupongeza UWT, kwa kuja na wazo la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, kwa kuandaa mkutano mkubwa Zanzibar uliofanyika Novemba 20, mwaka huu kwa mafanikio makubwa.
Aliongeza kuwa mikutano na makongamano kadhaa ambayo yamekuwa yakifanywa na umoja huo, yamekuwa yakimfariji kwa kiasi kikubwa Rais Samia na kuona kwamba Chama, wanachama, jumuiya zake na wananchi wote wa Tanzania, wanaendelea kumuunga mkono.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Katibu Mkuu mpya wa Umoja huo, Phillis, kwa kushika wadhifa huo na kueleza kwamba ana matumaini makubwa kwamba nafasi hiyo ataifanyia kazi ipasavyo kutokana na kuufahamu utendaji wake wa kazi.
Awali, Mwenyekiti wa UWT, Gaudentia Kabaka, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza vyema majukumu yake ya Urais, ambapo amekuwa akifanya vizuri tangu kuchaguliwa kwake.
Katika maelezo yake, Mama Kabaka alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba UWT, utaendelea kumuunga mkono pamoja na kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Chama tawala CCM, katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua na kuendelea kupata maendeleo endelevu.
Miongoni mwa viongozi wa UWT waliofika Ikulu juzi ni Mwenyekiti Mama Gaudentia Kabaka, Makamu Mwenyekiti Thuwayba Kisasi, Katibu Mkuu Phillis Nyimbi na Naibu Katibu wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo.
Na MWANDISHI WETU, Zanzibar