RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Ireland kwa kuwa tayari kuiunga mkono serikali ya awamu ya nane, katika kuimarisha sekta za maendeleo, utalii na uchumi wa buluu.
Ameyasema hayo Ikulu alipokutana na Balozi wa Ireland nchini, Mary O’Neil na kufanya mazungumzo yaliyojikita katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inathamini sana uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya pande mbili, akaipongeza Serikali ya Ireland kwa utayari wake wa kusaidia maendeleo ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliipongeza Ireland kwa kutoa nafasi za masomo ya elimu ya juu kwa vijana wa Zanzibar na matarajio makubwa, watakapomaliza masomo yao, watatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar.
Aidha, alisema katika kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano, amejipanga zaidi kusaidia maendeleo ya wanawake na kuwawezesha wakiwemo wajasiriamali kuona wanapiga hatua kubwa ya maendeleo na kupambana na umasikini.
Aliyataja maeneo ambayo serikali imejipanga kuwasaidia wanawake kuwa ni kilimo cha mwani ambacho wakulima wake kwa asilimia kubwa ni wanawake, ili kuona wanapata soko la uhakika wa uwekezaji wa viwanda vitakavyosanifu na kuongeza thamani ya zao hilo.
”Katika mipango ya miaka mitano tumejipanga kuwawezesha wanawake kuona wanapiga hatua kubwa katika kilimo cha mazao ya baharini kikiwemo mwani kwa kujenga viwanda vitakavyosarifu na kuongeza thamani ya zao hilo,” alisema.
Awali, Balozi Mary, alieleza kufurahishwa na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaunganisha wananchi katika serikali ya umoja wa kitaifa ambayo imeondoa uhasama wa kisiasa na wote kuwa kitu kimoja.
Alisema matarajio yake makubwa ni kuimarishwa kwa maridhiano ya kisiasa hatua ambayo itafungua milango ya uwekezaji na maendeleo katika sekta mbalimbali.
Balozi Mary alikubali kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii huku akitaka juhudi za kuimarishwa mazingira maeneo ya fukwe na kuwa kivutio kizuri.
Aidha, alisema nchi yake inaunga mkono uchumi wa buluu na kuona wananchi wananufaika na rasilimali za baharini ya kukuza uchumi na maendeleo ya taifa.
”Nipo tayari kuwa balozi wa kuutangaza utalii wa Zanzibar baada ya kuvutiwa na kuridhishwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi katika sekta hiyo na kuhakikisha tunaunga mkono uchumi wa buluu ambao lengo lake ni kulinda rasilimali za baharini na kuwanufaisha wananchi moja kwa moja,” alisema.
Na Waandishi Wetu, Zanzibar