RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, amekutana na uongozi wa Kampuni ya ‘International Holding Company (IHC) yenye makao yake Abu Dhabi na kuainisha fursa zinazoambatana na uwekezaji wa Uchumi wa Buluu, ikiwemo ya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Amezitaja fursa nyingine ni uvuvi mkubwa katika bahari kuu, ujenzi na kuzifanyia matengenezo meli za uvuvi, ujenzi wa bandari kubwa zitazoweza kuhimili meli kubwa za mizigo.
Dk. Mwinyi alikutana na uongozi wa kampuni hiyo kubwa katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E) na ya pili kwa nchi za Magharibi katika mkutano uliofanyika ukumbi wa kampuni hiyo ilioko Mjini Abudhabi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza kwa undani wawekezaji hao wa kampuni ya IHC fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu na kuwaalika kuja Zanzibar huku Abu Dhabi ikiahidi kuleta wawekezaji wa kigeni.
Dk. Mwinyi alisema kuwa, Zanzibar kwa sasa inahitaji wawekezaji makini huku akieleza moja ya fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu ni uwekezaji katika visiwa vidogo vinavyofikia 53 katika bahari ya Zanzibar.
“Fursa nyingine zinazoambatana na uwekezaji wa Uchumi wa Buluu ni pamoja na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, uvuvi mkubwa katika bahari kuu, ujenzi na kuzifanyia matengenezo meli za uvuvi, ujenzi wa bandari kubwa zitazoweza kuhimili meli kubwa za mizigo,” alisema.
Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa, yote hayo yatafanikiwa iwapo kutakuwa na miundombinu mizuri katika huduma za kijamii na kuwaeleza wawekezaji hao umuhimu wa kusaidia huduma za kijamii za elimu na afya na kuanzisha mikakati maalumu ya kiuchumi
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Shariff Ali Shariff, akitoa mwelekeo wa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji hao, aligusia hali ya watalii ilivyo Zanzibar, ambapo licha ya ugonjwa wa Uviko- 19, iliendelea kupokea watalii 39,512 kati ya Januari hadi Desemba, mwaka jana.
Alieleza kuwepo kwa fursa za kuwekeza katika kuchakata bidhaa za baharini, ujenzi wa boti za uvuvi na kuzifanyia matengenezo.
Pia, ujenzi wa mji mwingine utakaoitwa Zanzibar Marina City na kusaidia kilimo cha mwani.
Alieleza ipo haja kwa wawekezaji hao kuisaidia Zanzibar kuwa na kituo cha kukuza vipaji kwa michezo mbalimbali hali itakayoipaisha Zanzibar katika sekta ya michezo.
Alibainisha kuwepo kwa hekta 6,000 za ardhi inayohitaji kuendelezwa eneo la Makurunge, ardhi ambayo ni mali ya Zanzibar na inafaa kwa ajili ya kilimo.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje, Sheikh Shajkboot Nahyan Al Nahyan, walizungumza uhusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia ufunguzi wa Ubalozi Mdogo wa (U.A.E) Zanzibar na kurejesha huduma za ndege za U.A.E na kufanya safari zake Zanzibar.
Ziara ya Rais Dk. Mwinyi ilikamilika jana, alitarajiwa kuondoka Abudhabi jioni na kurejea Zanzibar.
NA MWANDISHI MAALUMU, ABUDHABI