RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ili taifa liwe na amani ni lazima kila mwananchi apate haki zake za msingi.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati wa sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya Askofu Mhashamu wa Kanisa Katoliki, Augustine Shao, iliyofanyika Uwanja wa Amani, Jijini Zanzibar.
Alisema ili taifa liwe na amani ni vema likahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi na kuahidi kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazolikabili kanisa.
Rais Dk. Mwinyi aliwataka viongozi wote wa dini katika madhehebu tofauti kuwa waadilifu kwa kigezo hatua hiyo itawaletea sifa na kuwajengea imani waumini wao.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sera ya Uchumi wa Buluu na utekelezaji wake, Dk. Mwinyi alisema serikali imegawa dhana hiyo katika sekta kuu tano, ambazo ni utalii, bandari, biashara na usafirishaji, uvuvi/mwani, mafuta na gesi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, utalii ni mhimili wa uchumi wa taifa, ambapo asilimia 30 ya pato la taifa linategmea utalii huku akibainisha malengo ya serikali ni kutumia vema rasilimali za bahari katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Dk. Mwinyi alisema kilimo cha mwani na uvuvi ni eneo linalochukua thuluthi mbili ya watu, hivyo serikali imeweka mkazo katika uimarishaji wa zana za uvuvi, ili kuimarisha uzalishaji na kuwaondolea wananchi umasikini.
Aliongeza kuwa serikali imeanzisha ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mangapwani itakayohusisha bandari tofauti kwa lengo la kuongeza pato la taifa.
Dk. Mwinyi alisema eneo lingine lililoko katika sekta hiyo ni mafuta na gesi na kubainsiha kiwango kikubwa cha gesi kilichokwisha kugunduliwa na wataalamu hadi sasa.
Alisema biashara na usafirishaji baharini ni neo ambalo bado halijafanyiwa biashara ya kutosha na kusema serikali ina azma ya kuimarisha biashara baharini ili kuchochea uchumi wake.
Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini ikiwa ni utamaduni uliozoeleka wa kuishi kwa amani na kuvumiliana miongoni mwa watu wenye imani tofauti za kidini.
Alisema Zanzibar ina historia ya muda mrefu ya wananchi wake kuishi kwa kuvumiliana kidini, jambo linaloiletea sifa kubwa nchi, sambamba na kuliwekea Taifa msingi muhimu wa Umoja.
Dk. Mwinyi alipongeza uamuzi wa Kanisa Katoliki Zanzibar kwa ushirikiano na viongozi wengine wa dini katika Kamati ya Kitaifa ya Amani inayojumuisha madhehebu tofauti ya Dini, na kusema mashirikiano hayo yanatoa nafasi kubwa ya kuimarisha umoja wa taifa katika kushajiisha maendeleo na ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, serikali inathamani mchangao wa viongozi wa kidini katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo, na kubainisha azma ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazohusu masuala ya ajira, usafirishaji wa binadamu, ukwepaji kodi pamoja na uimarishaji wa huduma za wagonjwa wanaoishi Kituo cha wazee Welezo.
Dk. Mwinyi alisema anatambua mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kuwahimiza waumini juu ya utii wa sheria na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya udhalilishaji, huku akipongeza taasisi za kidini kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili na ustawi wa jamii.
Mbali na hayo, alipongeza taasisi za kidini katika uimarishaji wa huduma za kijamii,ikiwemo uanzishaji wa skuli zilizo chini ya madhehbu ya dini, ujenzi wa vituo vya afya na kutoa huduma bila ya ubaguzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na viongozi na kuahidi kuendeleza mashirikiano na viongozi na waumini wa dini hiyo bila ubaguzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa, alisema serikali itaendelea kusimamia na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, hususan katika suala la imani na kuabudu.
Awali, Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mhashamu Askofu Shao pamoja na mambo mengine aligusia uwepo wa changmoto zinazolikabili kanisa na waumini wake.
Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Mahamoud Mussa alimsifia Askofu Shao kuwa mtu mpole , mwenye tabia njema pamoja na busara, hali inayomuwezesha kumudu kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Mozine Richard akitoa salamu kutoka kwa Papa, alitoa pongezi kwa Askofu Shao kwa kazi ya utume uliotukuka kwa kondoo wake katika kipindi hicho cha miaka 25.
NA HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR