RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameitaka Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kumpelekea taarifa za watendaji watakaobainika kuchelewesha kujaza fomu za tamko la viongozi, ili wachukuliwe hatua.
Agizo hilo alilitoa alipozungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili ya viongozi wa umma na utawala bora, yaliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdull Wakil.
”Nileteeni majina ya viongozi wanaochelewesha kujaza fomu za tamko la mali na madeni katika utumishi wa umma, viongozi wa aina hiyo ni wazembe na ndiyo wale unaowapa majukumu ya kazi wanashindwa kuleta ufanisi au kuchelewesha majukumu,” aliagiza.
Alisisitiza serikali ya awamu ya nane imejipanga kutekeleza dhana ya utawala bora kwa vitendo, ambapo viongozi wa umma na watumishi wake wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria kwa kujaza fomu za tamko la mali na madeni.
Alifafanua kuwa kujaza fomu ya tamko la viongozi ikiwemo mali na madeni ni sehemu ya kujitathmini kwa viongozi kwa kiasi gani wametekeleza dhana ya utawala bora na majukumu waliyokabidhiwa na taifa katika uaminifu.
Rais Dk. Mwinyi alitoa mfano mwaka huu, fomu za viongozi wa watumishi wa umma zilizowasilishwa katika tume hiyo ni 289.
Aidha aliitaka tume hiyo kufuatilia mwenendo wa viongozi wa umma na kumpelekea majina ya watendaji watakaobainika kutumia vibaya madaraka waliyopewa ikiwemo kuwaonea wananchi.
Aliahidi kuifanyia kazi taarifa ya tume hiyo itakayofikishwa kwake ikiwemo matukio ya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi.
Rais Dk. Mwinyi alisema zipo taarifa za baadhi ya watendaji wa serikali kukwamisha kwa makusudi utendaji wa ufanisi wa kuanza kazi kwa mfumo wa kielektroniki katika makusanyo ya mapato ya serikali.
Pia alisema wapo watendaji ambao kwa makusudi wanaokwamisha utendaji kazi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kukwepa kutoa taarifa sahihi na fedha na ukaguzi wake.
”Tuwafichue watendaji wanaokwamisha kuanza kazi kwa mifumo ya ukusanyaji wa fedha kwa njia ya kielektroniki ili kuingiza mapato ya nchi na wale wanaokataa kutoa ushirikiano na Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu ukaguzi wa hesabu za serikali,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza Mamlaka ya Kupambana Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA) kwa kufichua tuhuma mbalimbali zinazohusu rushwa na kuzifanyia kazi na kuitaka kuongeza kasi ya mapambano hayo.
Akitoa takwimu, Rais Dk. Mwinyi alisema tuhuma 289 za rushwa na uhujumu wa uchumi ziliwasilishwa katika mamlaka hiyo kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka huu huku kesi 29 zikifishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
”Ongezeni kasi katika kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi…mnafanya kazi nzuri ingawa idadi ya kesi zilizofikishwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ni ndogo sana,” alisema.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora, Haroun Ali Suleiman, aliitaka tume hiyo kutekeleza majukumu yake vyema ikiwemo kuwabana viongozi wanaokikuka maadili ya umma na kutoa taarifa taasisi husika.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Assa Ahmed Rashid, alizitaja miongoni mwa kazi walizofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kuwa ni kutoa elimu na kazi ya tume kwa watendaji wapya wa serikali na kufahamu majukumu yake.
NA KHATIB SULEIMAN, ZANZIBAR