RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza serikali anayoiongoza ina lengo la kuhakikisha inajenga uchumi imara, utakaoleta maendeleo kwa wananchi wote.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo, alipozungumza na viongozi na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, waliofika Ikulu Zanzibar kumpongeza.
Alieleza siasa ni uchumi na siasa ikiwa nzuri na uchumi huimarika, hivyo juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na serikali anayoiongoza katika kuhakikisha kunajengwa uchumi imara na madhubuti.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wazee hao mipango na mikakati ya kuimarisha sekta za maendeleo ili uchumi uzidi kuimarika na vijana kupata ajira na serikali kupata mapato.

Alisema jambo la msingi ni kuwepo amani na utulivu, juhudi ambazo zimechukuliwa katika kuhakikisha linafanyika.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendeleza utamaduni wa kukutana na kiongozi walioko madarakani kwa azma ya kuzungumza na kubadilishana mawazo.
Alitoa shukrani kwa dua wanazofanya wazee hao mara kwa mara kwa viongozi na nchi yao na kuwasisitiza kuendeleza utaratibu huo.
Aliwaeleza wazee hao juhudi zinazochukuliwa na serikali anayoiongoza za kuhakikisha jengo la kihistoria la Beit al Jaib, linajengwa upya na kurudi katika hadhi ya asili, ujenzi ambao unatarajiwa kuanza Febuari, mwakani.
Pia, Rais alieleza hatua za serikali kuhakikisha huduma za afya zinaimarika ikiwemo kuanzisha huduma za Bima ya Afya ili iwe rahisi kupatikana kwa huduma hiyo.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa kuijenga upya nyumba ya Kijangwani iliyokuwa Ofisi ya ASP ambayo kwa sasa imebomoka kwa azma ya kuhakikisha historia haipotei.

Akisoma tamko la Baraza la Wazee, Mzee Haji Machano, alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 na ushiriki kampeni alizofanya.
“Umekemea rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, umerekebisha mfumo mzima wa elimu na kukarabati utawala, umekemea ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, umechukizwa sana na uingizaji na utumiaji dawa za kulevya nchini na umeunda chombo cha udhibiti na ufuatiliaji, umepanua uchumi wa buluu na umewaita wawekezaji”,ilisema sehemu ya tamko hilo.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na wawekezaji wa kampuni ya sukari Kilombero wakiongozwa na Balozi Ami Ramadhan Mpungwe, katika mkutano wenye lengo la kupanua shughuli na uzalishaji wao, ambapo aliwapongeza kuamua kufanya mkutano huo Zanzibar.
Na MWANDISHI WETU