RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuchagua viongozi madhubuti wenye uwezo wa kukivusha Chama katika uchaguzi mkuu wa 2025.
Dk. Mwinyi ambae ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, aliyasema hayo wakati akitoa salamu kwa wanachama na viongozi wa tawi la CCM Kilimani, baada ya kukamilisha upigaji kura katika uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa tawi hilo ngazi ya Tawi.
Alisema jukumu kubwa la Chama cha siasa ni kushika dola, hivyo kuna umuhimu wa wanachama wa CCM, kuchagua viongozi madhubuti wenye uwezo wa kukivusha chama katika uchaguzi mkuu ujao wa 2025.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwepo changamoto mbalimbali zinazokabili chaguzi za Chama ambapo katika baadhi ya maeneo, viongozi wanaogombea hubainika wakiwa wagawaji wa fomu za kupigia kura, jambo ambalo si sahihi.
Hivyo, aliwataka wale wanaotetea nafasi zao kukaa pembeni na kazi hizo zifanywe na watu wengine.
Dk. Mwinyi aliwapongeza wanachama wa tawi hilo kwa kufanya uchaguzi kwa kufuata utaratibu unaokubaliwa na kuwataka waendelee hivyo katika chaguzi zote zitakazofuatia.
Alisema chaguzi ngazi za mashina na matawi ni muhimu katika ustawi wa Chama kwa kuzingatia kwamba, ndiko kwenye mitaji ya watu.
Uchaguzi huo umewashirikisha wajumbe wapatao 182, ambapo jumla ya nafasi sita zimegombewa, ikiwemo ya Mwenyekiti wa CCM tawi, Katibu wa CCM tawi, Katibu wa Siasa na Uenezi, wajumbe watano wa mkutano mkuu wa CCM wadi, wajumbe 10 wa mkutano mkuu wa CCM tawi na mjumbe mmoja wa mkutano mkuu wa jimbo na wilaya.
Wakati huo huo, Dk. Mwinyi alipata fursa ya kusalimiana kisha kumjulia hali mwanasiasa mkongwe Asha Simba Mwakwega.
WANDISHI MAALUMU