RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwepo wataalamu wa sheria wenye ujuzi ni muhimu katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini.
Dk.Mwinyi amesema hayo katika hafla ya ufunguzi wa jengo la Mahakama Kuu, lililopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema juhudi za serikali za kuimarisha majengo na upatikanaji wa vifaa, hazina budi kuambatana na utoaji wa mafunzo, ambapo wafanyakazi wa kada ya sheria watapata fursa ya kushiriki ndani na nje ya nchi.
Alisema wataalamu wa sheria wanapaswa kuishauri serikali masuala muhimu ya maendeleo, ikiwemo uandaaji wa mikataba na taasisi za kimataifa.
Alieleza kukamilika ujenzi wa jengo hilo ni hatua muhimu katika kutekeleza azma ya serikali ya kuweka mazingira bora ya kufanyia kazi katika utumishi wa umma, kama ilivyobainisha katika mkakati wa mabadiliko katika Utumishi wa Umma wa 2010.
Dk. Mwinyi alisema kwa miaka mingi Mhimili wa Mahakama ulikuwa ukikabiliwa na changamoto ya ufinyu wa nafasi na uchakavu wa majengo, huku mengi yakiwa yamerithiwa kutoka kwa wakoloni, ikiwemo Jengo la Mahakam Kuu lililopo Vuga, Jijini Zanzibar.
Alisema serikali itaendelea na dhamira ya kujenga majengo ya kisasa na kuweka vifaa vya kufanyia kazi vinavyoendana na mabadiliko, mahitaji ya wakati uliopo.
Alitoa wito kwa watumishi wa umma kutunza vifaa na mejengo yaliyopo katika maeneo yote ya kazi kwa kutambua kuwa ni mali ya wananchi.
Dk. Mwinyi aliagiza uongozi wa Mahakama kuendelea kulitunza jengo lililopo Vuga, huku akisisitiza azma ya serikali ya kulifanya eneo la Mji Mkongwe kutumika kwa shughuli za utalii.
Alimshukuru Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein kwa maono na kuja na wazo la ujenzi wa jengo jipya la Mahakama, na kusema uamuzi wake ulikuwa ni wa kimaendeleo.
Akigusia changamoto zinazoihusu Mahakama, aliagiza uongozi wa Mahakama kuendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili mhimili huo.
Alisema ujenzi wa jengo hilo ni mikakati ya serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi, na kubainisha uwezo wa serikali wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali zake wenyewe.
“Ujenzi wake umezingatia mahitaji ya wananchi kwa namna tofauti, ikiwemo upatikanaji wa huduma za benki na watu wenye mahitaji maalumu…..ni imani yangu kuwa watendaji watakaofanyakazi katika jengo hili watafanyakazi kwa kuzingatia uwajibikaji na uadilifu”, alisema.

Kaimu Jaji Jaji Mkuu Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, alisema ujenzi wa jengo hilo umetokana na jengo la Mahakama Kuu lililopo Vuga kuwa na changamoto nyingi, ikiwemo ufinyu wa Ofisi, kutokuwa rafiki kwa jamii ya watu wenye ulemavu na mfumo wa Tehama.
Alisema wakati wa kipindi cha vikao vya Mahakama ya Rufani, baadhi ya Majaji hulazimika kuchukua likizo ili kupisha Majaji wa Mahakama ya Rufani kuendelea na majukumu yao.
Alisema changamoto kubwa inayokabili Mahakama katika usikilizaji wa kesi za udhalilishaji ni mashahidi kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, huku baadhi ya nyakati wahusika wa kesi hizo wakibainika kufunga ndoa.
Kaimu Jaji Ramadhan, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kufikiria uwezekano wa kujenga jengo jipya la Mahakama Kisiwani Pemba, kufuatilia lile liopo hivi sasa katika eneo la Kichungwani Chakechake kuwa katika mazingira yasiofikika kirahisi kutokana na changamoto ya ukuaji wa mji.
Aidha, Waziri wa Nchi, Katiba, Sheria, Utumishi wa Uma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisisitiza haja ya watendaji wa Mahakama kuwajibika ipasavyo kiutendaji ili kwenda sambamba na mazingira halisi ya jengo hilo.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma alisema ujenzi wa jengo hilo ni kielelezo cha dhamira ya serikali katika kuhakikisha mhimili wa Mahakama unawezeshwa, hivyo akaiomba serikali kuendelea na uwezeshaji huo hadi ngazi za chini.
Alisema jengo hilo ni zuri na linatoa matumaini katika utoaji wa haki, hivyo akabainisha mtihani unaowakabili watendaji wa mhimili huo katika kuhakikisha matumaini ya wananchi yanafikiwa, kuendana na mahitaji ya ujenzi wa Uchumi wa Buluu.

(Picha na Ikulu)
Aliwataka Majaji na Mahakimu kujiwekea utaratibu wa kuwajibika na kuhakikisha jengo hilo linaendana na kasi ya maendeleo ya Zanzibar, huku akiahidi Mahakama Kuu ya Tanzania kuendelea kushirikiana kikamilifu na Mahakama Kuu ya Zanzibar.
Mapema, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kai Bashiru Mbarouk alisema Jengo hilo la Mahakama Kuu lililopo Tunguu limegharimu sh. bilioni 16.8, ambapo fedha zote hizo kwa asilimia mia moja zinatoka katika mfuko wa serikali.
Alisema jengo hilo lililojengwa na Kampuni ya Advent Construction Limited limejengwa katika eneo la ekari 4.3 likiwa la ghorofa nne ambapo msingi wake ni wa ghorofa saba, ambapo ujenzi wake umezingatia mambo mbalimbali kuhimu ikiwemo usalama.
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR