RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati umefika Zanzibar kuanzisha kituo cha utatuzi wa migogoro ya kibiashara.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kwenda sambamba na hatua ya serikali ya kuvutia wawekezaji katika miradi mikubwa.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, hafla iliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni, Jijini Zanzibar.
“Nadhani tunalazimika sasa kutunga sheria ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara, ili tukishaipata tuwe na chombo au kuanzisha kituo cha utatuzi wa migogoro ya kibiashara hapa Zanzibar,” alisema.
Dk. Mwinyi alisema amezingumza na Mwanasheria wa Serikali, hivyo ni matumaini yake miradi mikubwa inayofanyika Zanzibar migogoro yake haitapelekwa mahakamani.
“Hakuna sababu ya hilo, kwa kuwa Nairobi wamefanya, Kigali wamefanya na sioni kwanini Zanzibar tusifanye jambo hilo,” alisema na kusisitiza ni vyema kuwepo kwa sheria na mifumo ya utoaji haki itakayovutia wawekezaji na kuweka vitega uchumi vyao nchini na kutoa ajira kwa wananchi.
USIMAMIZI WA UTOAJI WA HAKI
Dk. Mwinyi alieleza kuwa ni muhimu viongozi katika sekta zote kuzingatia na kusimamia vizuri utoaji wa haki, ili imani ya wananchi kwa serikali na vingozi iongezeke.
Alisisitiza utoaji wa haki kwa misingi ya sheria na usawa inaepusha jamii na migogoro isiyokuwa na lazima na inawahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo.
“Kwa kutambua hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuboresha taasisi na mifumo ya utoaji wa haki, ili kuimarisha kasi ya maendeleo na ujenzi wa nchi,” aliahidi.
Pia, aliwataka wataalamu wa sheria katika sekta ya umma na binafsi, kujiendeleza kitaaluma na kushiriki katika mafunzo mbalimbali hususan maeneo mapya ya sheria yanayohitajika kutekeleza mageuzi ya kiuchumi yanayopangwa.
Alisema utaalamu wa sheria lazima uwe katika maeneo yote ili kukidhi mahitaji ya wawekezaji na washiriki wa maendeleo waliopo nchini.
Aliongeza kwamba mifumo ya sheria iliyopo ni lazima iwe chachu ya kuwaondolea wananchi ugumu wa maisha na kuwawezesha kujiajiri wenyewe kwa lengo la kuchangia maendeleo ya nchi.
Alisema siyo jambo linalopendeza kwa wananchi na wawekezaji kuchukua muda mrefu mahakamani na katika taasisi nyingine za utoaji wa haki.
Dk. Mwinyi alieleza kumekuwepo malalamiko mengi yanayowasilishwa kwake kupitia Mtandao wa Sema na Rais, kuhusu ucheleweshaji wa utoaji haki unaofanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi za serikali, hivyo aliwahimiza viongozi kuongeza bidii katika usimamizi wa haki za wananchi kwa kuzingatia sheria.
Rais Dk. Mwinyi alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha mazingira ya utoaji wa haki, ikiwemo kufanikisha ujenzi wa majengo ya kisasa ya taasisi hizo na kuzipatia nyenzo kwa kadri hali ya fedha na uchumi inavyoruhusu.
USHIRIKIANO MAHAKAMA YA ZANZIBAR NA TANZANIA
Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania, Mahakama ya Zanzibar na taasisi zote za utoahji haki nchini na kubainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano.
Maeneo hayo ni matumizi ya lugha ya Kiswahili, mifumo ya TEHAMA, mafunzo kwa watumishi, namna bora ya kupambana na dawa za kulevya na usuluhishi wa migogoro.
Dk. Mwinyi alimpongeza Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Rmadhan Abdalla kwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika kipindi kifupi, na hivyo akawataka watendaji na watumishi wa mhimili huo kuunga mkono juhudi hizo.
Aliushukuru uongzi wa Mahakama ya Tanzania kupitia Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuanza kuisaidia Mahakama ya Zanzibar.
MATUMIZI YA LUGHA YA KISWAHILI MAHAKAMANI
Dk. Mwinyi alihimiza utumiaji wa lugha ya Kiswahili katika Mahakama za Zanzibar, ili kuwasaidia wananchi kutopoteza haki zao kwa kutokuelewa lugha ya Kiingereza inayotumika.
Alisema lugha ni nyenzo muhimu katika usimamizi wa haki, ambapo upo uwezekano mkubwa watu kupoteza haki zao kwa sababu ya kutoelewa lugha ya kigeni inayotumika.
“Tuhakikishe uendeshaji wa mashauri na uandishi wa sheria unafanywa zaidi kwa lugha ya kiswahili badala ya lugha ya kigeni,” alisema.
KAIMU JAJI MKUU ZANZIBAR
Awali, Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla alisema kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Usimamizi wa Haki ni Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii”, imezingatia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali katika kujenga Uchumi wa Buluu.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa dhana hiyo, kumekuwa na mwamko mdogo kwa wafanyabaishara wa Zanzibar kufungua kesi katika Mahakama ya Biashara.
Alisema katika mwaka 2021 kulikuwa na mashauri 11 pekee yalioripotiwa mahakamani, hivyo akatoa ahadi ya kuendeleea kuitangaza Mahakama hiyo kwa jamii ili itumike kikamilifu.
Aliyataja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa haki ni kuwepo kwa mahakimu sita wanaosikiliza kesi za udhalilishaji na Mahakimu watatu wa kusikiliza kesi za dawa za kulevya.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu Mahakimu hao hawapangiwi kesi za aina nyingine, huku muda wa kusikiliza kesi ukiongezwa hadi saa 11, ikiwa ni hatua ya kumaliza mashauri hayo kwa haraka na kutoa fursa kwa wananachi kufanya kazi nyengine.
Kuhusu ongezeko la mahabusu katika Magereza Kisiwani Pemba, Kaimu Jaji Mkuu alisema amewaagiza Mahakimu kutoa dhamana kwa mahabusu wa kesi zote zenye dhamana na kuongeza nguvu ya usikilizaji kwa kesi ambazo hazina dhamana, huku Mahakama ikizingatia mfumo wa kutekeleza adhabu katika jamii.
Jaji Khamis alitoa wito kwa jamii kuondokana na tabia iliyojitokeza ya uwepo wa ushirikiano kwa lengo la kuharibu kesi hususan za udhalilishaji kwa wadhuriwa wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi miaka 17.
WAZIRI WA KATIBA
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria , Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema kuna mabadiliko ya kiutendaji katika shughuli za kimahakama na kubainisha kuwepo ushirikiano mkubwa kwa watendaji wa usimamizi wa haki, ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Jeshi la Polisi, Mahakama na Mawakili.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji alisisitiza umuhimu wa dhana ya Uchumi wa Buluu kuzungumzwa mara kwa mara.
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Salma Ali Khamis alisema changamoto kubwa inayokwaza utekelezaji wa usimamizi wa haki ni ile ya wananchi kushindwa kufika Mahakamani kutoa ushahidi hususan katika kesi za udhalilishaji, hivyo akabinisha umuhimu wa kuwepo mabadiliko ya kiutendaji na kisera.
Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar, Dk. Slim Abdalla aliishauri serikali kuweka mkazo katika utatuzi wa migogoro ya kiuchumi, kifedha na kibiashara na kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kuanzisha kituo cha utatuzi wa migogoro ya kibiashara.
Siku ya Sheria Zanzibar huadhimishwa kila ifikapo Februari 2 kila mwaka, ikiashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama.
NA HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR