RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Magazeti ya Serikali kuendelea kuwa wabunifu katika kuandika habari na hasa zile zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya gazeti la Zanzibar Leo, zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, Kiembesamaki, mjini Zanzibar.
“Kwa mnasaba huo, uongozi na wafanyakazi wa gazeti hili mnapaswa kufanyakazi zenu kwa weledi ili kuwafanya wananchi na wasomaji wote waweze kuliamini Gazeti letu kuwa ndicho chombo kinachotoa taarifa sahihi zilizoandikwa kwa umakini na zilizofanyiwa uchunguzi,” amesema Dk. Mwinyi.
Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Magazeti kwenda na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo imeongeza ushindani katika sekta ya habari kama ilivyo katika sekta nyingine.
Ameongeza kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya gazeti la serikali la Zanzibar Leo ni kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na zenye ubora, ili kukabiliana na ushindani uliopo hasa kutoka kwa magazeti ya kampuni binafsi.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alivikumbusha vyombo vya habari vya serikali kuwa mdomo wa serikali, kwa hivyo vinawajibu mkubwa wa kuisemea.
Amesema kuwa kutokana na kukua kwa tasnia ya habari na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, wapo baadhi ya watu huitumia vibaya fursa ya uhuru wa habari kwa kupotosha, hivyo vyombo vya habari vya serikali vina jukumu la kuchukua hatua haraka za kuelezea usahihi wa taarifa kwa kutuma hoja, vielelezo na ufafanuzi wa jambo husika.
Rais Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwapongeza mawaziri wote kwa kutoa taarifa za kina juu ya utekelezaji wa majukumu ya wizara zao katika maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi na kutoa wito kuwa waendelee na utaratibu huo na usiwe katika kipindi cha sherehe pekee.
Aidha, aliwataka viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali kuvitumia vyombo vya habari vya umma na vya binafsi kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwa umma, kubainisha changamoto pamoja na kueleza watakavyokabiliana na changamoto hizo.
Alieleza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi na watendaji wa Shirika la Magazeti katika kuimarisha mazingira ya kufanyakazi pamoja na kuzifanyia kazi changamoto wanazo zikabili, huku akitumia fursa hiyo kutoa agizo kwa taasisi za serikali na sekta binafsi zinazodaiwa na shirika hilo kulipa madeni yao ili shirika liweze kuendesha shughuli zake.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya saba kwa kuwekeza fedha nyingi katika kuimarisha sekta ya habari hapa Zanzibar.

Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alitoa pongezi kwa Rais mstaafu wa awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume, kwa kuwa mwasisi wa gazeti hilo pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuliendeleza na kuipa msukumo mkubwa sekta ya habari kupitia vyombo vya umma, likiwemo gazeti hilo.
Sambamba na hayo, Waziri Tabia alitoa pongezi kwa Rais Dk, Mwinyi kutoka kwa wadau mbalimbali kutokana na uamuzi wa kuzungumza na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi.
Pia, Waziri Tabia alitumia fursa hiyo kuwa pongeza wafadhili wote walio fadhili shughuli hiyo ambayo ili fana.
Kwa upande wake Mhariri Mtendaji wa gazeti la Zanzibar Leo, Ali Haji Mwadili akisoma risala ya kitaalamu ya Shirika la Magazeti ya Serikali alisema gazeti hilo lilianzishwa Januari 12 2022 na Rais mstaafu wa awamu wa sita Amani Abeid Karume likichukua nafasi ya gazeti la Nuru kwa lengo la kusambaza sera za serikali.
Aliongeza kuwa, kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Habari na uchumi wa buluu” alisema yenye lengo la kukumbusha umuhimu wa na mchango wa sekta ya habari katika maendeleo na mafanikio ya uchumi wa buluukwa kuwaelimisha na kuwahabarishawananchi.
Akieleza miongoni mwamafanikio mhariri mtendaji huyo alieleza kuwa ndani ya miaka 20 gazeti la Zanzibar Leo limezaa magazeti mengine manne ambayo ni Zanzibar Leo Jumaapili, Zasport, Zanzibar Mail pamoja na Zanzibar Leo wanawake, linalochapishwa kila mwisho wa mwezi, huku likipanua wigo wa usambazaji magazeti kwa mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha,alieleza changamoto zinazolikabili gazeti hilo ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za uchapishaji na usambazaji wa magazeti kutoka na kupanda kwa malighafi.
Alisema wakati mwingine wachapishaji hutaka faida kubwa ambapo kwa sasa asilimia 70 ya mapato ya shirika yanatumika katika uchapishaji.
Alisema kutokana na maendeleo ya kimtandao na mabadiliko ya tasnia ya habari, magazeti duniani yanahitaji kuendana na matakwa hayo, ambapo kwa sasa shirika lina jipanga kuimarisha mitandao ya kuendelea kuuza magazeti ya kwa njia ya mtandao.
Na MWANDISHI WETU