RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza haja kwa watendaji serikalini kubadilika na kutofanya kazi kwa mazoea ili mipango iliyopangwa itekelezeke.
Aliyasema hayo baada ya kusikiliza mada zilizowasilishwa na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Mafunzo ya Upangaji wa Vipaumbele, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya ‘Tony Blair’ na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.
Dk. Mwinyi amesema kuwa kazi iliyobaki mbele hivi sasa ni utekelezaji kwa kuwa hakuwa na shaka na utekelezaji kwa kuwa mipango ipo bali lengo ni kuimarisha Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, kilichobaki ni utekelezaji.
Rais Mwinyi alikumbushia kauli yake aliyoitoa siku aliyoyafungua mafunzo hayo kwa kusema kwamba hajaridhika na utendaji serikalini na kueleza kwamba hakusema hilo kwa kumnyooshea kidole mtu, bali alisema kutokana na hali halisi ilivyo kwa kuwa bado watendaji serikalini hawajawa wepesi katika kufanya mipango ya serikali itekelezeke.
Alisisitiza mabadiliko na kueleza kwamba kila mmoja ni vyema ajione kwamba ana wajibu wa Ofisi yake kutekeleza mipango iliyopangwa na haitokuwa vyema kiongozi kumaliza kipindi chake cha uongozi bila ya kuonyesha mradi hata mmoja aliotekeleza.
Alisema hawezi kusema amefanikiwa, bali atakuwa amefanikiwa kwa kwenda kazini tu, lakini hakufanikiwa kuonesha ama kuacha alama katika Ofisi yake na kusisitiza kwamba kila mmoja anapaswa kuonyesha alichokifanya pale atakapomaliza muda wake wa kazi.
Rais Dk. Miwnyi alisema hatokuwa tayari kusikia wawekezaji wanaokuja kuekeza wanazungushwa.
Alisema kwamba masuala ya uwekezaji yanataka fedha, hivyo si jambo la busara wawekezaji wakazungushwa kwani wenye fedha ni lazima wakapokewe vizuri na kuwakarishwa ili waweze kufanya kazi.
Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba bado kuna watu wanadhani kwamba urasimu ndio njia ya kufanyakazi na kusisitiza kwamba wakati umefika watu wabadilike.
“ …..bado kuna hali ya kutojali na hivyo ndipo niliposema kwamba siridhiki na utendaji wa Serikali…nyinyi mliokuwepo hapa ndio wakuu wa taasisi zetu…inawezekanaje upo katika kipindi chako cha uongozi kwa miaka mitano hata mtu mmoja hajakemewa…ina maana katika ofisi zetu hamna anayefanya kosa, hayo ndio yanayotufanya tushindwe kufanikiwa, ningependa kusikia kila mtu anachukua hatua ili kufanya ofisi zetu zifanye kazi vizuri zaidi,” alisisitiza Dk. Mwinyi.
Alisema anaamini semina hiyo itawasaidia watendaji kubadilika na wameshajua mipango na majukumu ya Serikali na lililobaki ni kwenda kupanga jinsi ya kuwezesha kifedha ili mipango hiyo iweze kutekelezeka.
Sambamba na hayo, alitoa pongezi kwa wadhamini wa mafunzo hayo pamoja na kuwapongeza viongozi wote waliopata mafunzo hayo, ambayo alisema yana umuhimu mkubwa na yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya Serikali.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kuhudhuria katika uwasilishwaji huo wa mada mbalimbali zilizotolewa na Makatibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kwamba mafunzo hayo yamewapa mwanga mkubwa wa kutekeleza mipango na upangaji wa vipaumbele vyake sambamba na kuyafanyia kazi maoni yake aliyoyatoa.
Awali, Makatibu Wakuu walipata fursa ya kuwasilisha mada zao na kueleza mipango kabambe waliyoipanga katika mafunzo hayo, ikiwemo mipango ya kuimarisha sekta ya uchumi wa Buluu, sekta ya utalii, sekta ya miundombinu pamoja na masuala ya kijamii.
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR