RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliondoka nchini Januari 16, 2022, kwenda Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (U.A.E), kwa ziara ya siku tatu.
Akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi aliagwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, dini na wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.
Ziara hiyo ya Rais Dk. Mwinyi inatokana na mwaliko maalumu wa kiserikali aliopewa na Mrithi wa Mtawala wa Abudhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E), Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.
Rais Dk. Mwinyi anatarajia kuanzia ziara yake hiyo nchini Abudhabi, ambako atahudhuria maadhimisho ya wiki Maalumu ya Kushajihisha Maendeleo endelevu inayoadhimishwa kila mwaka nchini humo tangu mwaka 2008 na kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi na serikali mbalimbali duniani utakaofanyika Dubai.
Katika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi, pamoja na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.