WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amezipongeza kampuni zaidi ya nane za Kitanzania zilizopo nchini Marekani kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania katika sekta ya uwindaji wa kitalii kwa kushiriki katika mkutano wa 50 wa mwaka wa uwindaji wa kitalii.
Mkutano huo wa 50 wa mwaka wa uwindaji wa kitalii ulioandaliwa na Safari International Club(SCI) umeanza leo Januari 21, 2022 na unaofanyika katika Jiji la Las Vegas, Nevada nchini Marekani
Akizungumza jijini humo, Dk. Ndumbaro amesema maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Tanzania zikiwemo kampuni na viongozi wa serikali kushiriki katika mkutano huo kujifunza na kuinadi Tanzania katika masuala ya uwindaji wa kitalii na nyanja za kimataifa
”Katika maonyesho haya zaidi ya kampuni 200 zinazofanya biashara ya uwindaji wa kitalii kutoka kila kona ya dunia yapo hapa yakiwemo kutoka bara la Ulaya,Amerika, Afrika, lakini nchi za Canada na Marekani yenyewe,” alisisitiza.
Dk. Ndumbaro amesema maonyesho hayo ni makubwa ambayo yanatoa fursa kwa nchi kujifunza sekta ya uwindaji wa kitalii kuwa ipo wapi sasa hasa kipindi hiki cha ugonjwa wa Uviko- 19.’’
“Mimi kama Waziri mwenye dhamana na utalii najisikia fahari kuona kampuni zaidi ya nane za Kitanzania zipo hapa zikiiuzaTanzania katika sekta ya uwindaji wa kitalii,”alisema.
Waziri huyo alisema kushiriki kwa kampuni hizo ni hatua nzuri na ni ushandi kuwa zinafanya vizuri na zinakubalika kimataifa ambapo alichukua fursa hiyo kukutana nao kwa pamoja na mmoja mmoja ili kubadilishana mawazo.
Alisema mazungumzo aliyoyafanya na kampuni hizo yamemfundisha mengi ikiwemo kuanza kuingalia sekta ya uwindaji wa kitalii kwa namna ya utofauti kabisa na kwamba,uwindaji ni sekta ya kipekee ambayo inaweza ikawa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kama itachukuliwa kwa uzito unaostahili
“Tumekubaliana tutaendelea kujipanga kushirikiana na kwa siku zilizobaki kuiuza Tanzania lakini muhimu zaidi kuongea na Waandaji wa maonesho haya na maonesho mengine ili katika safari ijayo Tanzania ishiriki kama nchi kwa umoja wake na kwa fursa kubwa zaidi ili kuuza utalii wa uWindaji” Alisema Dkt. Ndumbaro

Kwa upande wake, mmoja wa wanaoendesha biashara ya utalii wa uwindaji nchini ambaye yupo katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya Michel Mantheakis Safari, Michel Manteakis, alisema wamekuwa wakihudhuria kila mwaka na kupata faida kubwa ya soko kutoka kwa wateja wanaofika katika mikutano hiyo.
“Mikutano hii ni muhimu sana kuhudhuria, kwani tunakutana na wageni mbalimbali na bila kuhudhuria unakosa fursa kwani mawakala na wateja wanafika hapa.
“Hapa kuna washiriki wa kutoka nchi zote za Afrika,hivyo usipohudhuria mkutano huu utakosa soko. Hapa ndipo tunapokutana na wageni wetu tunapata faida ya kuendesha safari zetu, wateja na mawakala wanapata fursa ya kutufanyia usahili na pia wanaona jinsi tunayonadi bidhaa zetu,”alisema.
Mkutano huo ulioanza Januari 19, mwaka huu na ulifunguliwa rasmi juzi katika Jiji la Las Vegas, Nevada nchini Marekani ukiwa na lengo ya kuwakutanisha watunga sera na wafanya maamuzi katika ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili masuala ya kisera na kuendeleza sekta ya uwindaji.
NA MWANDISHI MAALUMU, LAS VEGAS, MAREKANI