MKOA wa Dodoma umepokea dozi 50,390 ya chanjo ya Uviko-19 aina ya Sinopharm baada ya kumaliza dozi ya awali.
Akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Afya ya Msingi kuhusu kinga na chanjo dhidi ya Uviko 19, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, alisema wameweka mikakati mahsusi kuhakikisha chanjo hiyo inamalizika kwa muda wa siku 28.
“Mkoa tumepokea chanjo mpya ya Sinopharm na tunatarajia kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupata chanjo ya Uviko-19, lengo tunataka kuona wananchi wanakuwa salama kama ilivyo azma ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Mtaka alisema chanjo hiyo ya Sinopharm imegawanywa katika wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma kuwarahisishia wananchi kutosafiri umbali mrefu kufuata chanjo.
Alisema wilaya ya Bahi imepewa dozi 5,000, Chamwino 6,000, Chemba 5,000, Dodoma Jiji 15,390, Kondoa 5,000, Kondoa Mji 4,000, Kongwa 5,000 na Wilaya ya Mpwapwa, wamepatiwa dozi 5,000.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatuma Mganga, alisema katika awamu ya kwanza walipokea dozi 50,000 za chanjo ya Uviko-19 hadi kufikia Oktoba 5, mwaka huu, walimaliza chanjo zote.
Alisema baada ya kumaliza walilazimika kuomba chanjo za ziada dozi 6,515 kutoka mikoa ya Geita dozi 5,000 na Iringa dozi 1515 ambapo hadi kufikia Oktoba 13 mwaka huu, wananchi 52,559 walikuwa wameshachanjwa.
“Katika chanjo tuliyopokea awamu ya kwanza tulifanya vizuri mbinu zile zilizotumika tukienda nazo naamini tutafanikiwa, lengo tunataka kila mwananchi afikiwe na huduma na ndio maana tuliweza kuongeza vituo vya kutolea huduma kutoka 28 hadi kufikia 381,”alisema.
Kwa upande wake, Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Dodoma, Dk. Francis Bujiku, alisema ili kupata chanjo kamili ya Uviko-19 ni lazima uchome dozi mbili ambapo dozi ya kwanza unachoma siku ya kwanza na ya pili huchomwa baada ya siku 21 tangu kuchoma dozi ya kwanza.
Alisema dozi ya pili haitakiwi kuchelewa kutolewa zaidi ya siku 28 na endapo mtu atapitiliza zaidi ya siku hizo itamlazimu kuanza upya kuchanja.
“Sinopharm ni moja ya chanjo za Uviko-19 zilizoidhinishwa na Shirika la Afya duniani (WHO) kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa huu. Chanjo hii ni mojawapo ya aina tano za chanjo ambazo zimeidhinishwa na serikali kutumika hapa nchini,”alisema.
“Chupa moja ya chanjo ya Sinopharm imejazwa dozi ya mtu mmoja ambapo chanjo hii hutolewa kwa mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea,”alisema.
Kwa mujibu wa Dk.Bujiku, chanjo hiyo ni kama chanjo nyingine ambapo mtu hupata maumivu ya sindano anapochoma, kujisikia uchovu na kuumwa kichwa.
Aliwataja watu wenye matatizo ya mzio wa mchanganyiko wa dawa iliyotumika kutengeneza chanjo hiyo kuwa hawatoruhusiwa kupata chanjo na mtu mwenye homa na joto la nyuzi 38.5 na kuendelea.
Na FRED ALFRED, DODOMA