HIFADHI ya Taifa ya Mikumi iliyopo wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, inafanya utafiti wa Faru kurudishwa katika hifadhi hiyo kwa lengo la kuhamaisha zaidi utalii.
Hayo yalisemwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Mathew Mombo, ambapo alisema kwa sasa wanyama maarufu waliopo katika hifadhi hiyo ni tembo, nyati, samba na chui ambao wamekuwa kivutio cha wageni.
Alisema historia inaonyesha mnyama faru aliwahi kuwepo katika hifadhi hiyo miaka ya nyuma, hivyo wameamua kufanya utafiti ili kubaini uwezekana wa mnyama huyo kurudishwa.
“Tumeona umuhimu wa kufanya utafiti mbalimbali kuhakikisha tunamrejesha mnyama faru na hapa tutaweza kuitangaza hifadhi zaidi na wageni wetu kuona wanyama wote watano wakubwa duniani,” alisema.
Alibainisha kuwa kuwepo kwa faru kutaweza kuitangaza Hifadhi ya Mikumu zaidi, hivyo kuongeza idadi ya watalii kutokana na kupatikana kwa wanyama wote maarufu wakubwa.
Mombo alisema mnyama faru pindi atakaporejeshwa katika hifadhi hiyo atajengewa uzio maalumu kwa ajili kuzoea mazingira yaliyopo na baadae ataachiwa.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi hiyo, Happiness Kiemi, alisema katika baadhi ya hifadhi ikiwemo Serengeti na Mkomazi wanyama maarufu watano wanapatikana, hivyo ni vyema wageni wanaotembelea nao wakapata fursa ya kumuona mnyama faru anapokuwa hifadhini.
Naye, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi, Idara Himasheria na Ulinzi Mkakati, Greyson Maro, alisema hifadhi imeimarisha mipaka na hakuna mtu anayeingia katika hifadhi au kufanya shughuli zozote katika mipaka bila kuwa na kibari.
“Tuna zaidia ya miaka mitano hakuna ujangili uliotokea mkubwa kwa wanyama kama tembo lakini kipindi cha zamani kilikuwa ni tatizo kwa wanyama hao,” alisema Maro.
Na WARIOBA IGOMBE