WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuanzia leo Agosti 17, 2021, gharama za urasimishaji kwa mwananchi ni sh. 130,000 tu, huku akionya baadhi ya watendaji wa wizara kuacha tabia ya kuzinyima kazi kampuni kwa sababu hazitoi rushwa.
Aidha, ameeleza kuanzisa sasa, suala la ulazima wa kuwa na hati miliki wananchi waishio mijini litakuwa kama zilivyo huduma nyingine za kijamii ikiwemo umeme na maji.
Hayo ameyasema jijini hapa leo wakati wa kikao chake na maafisa ardhi kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili hali ya urasimishaji nchini ambapo alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha namna ya kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
“Kwenye hili suala la urasimishaji hatufanyi vizuri sababu kuna baadhi ya watendaji wanapokea bahasha ili waipe kazi kampuni fulani na kuamua kubagua ambao hawajatoa bahasha na kusababisha michoro kulala licha ya kuwa kampuni zimeleta kazi wizarani mnazungusha watu hii tabia ya ubaguzi sio nzuri badilikeni kila mmoja apewe kazi ya urasimishaji,”amesisitiza.
Amesisitiza anataka kuona ndani ya miezi mitatu kila wilaya imefanya urasimishaji kama inavyotakiwa na watatembelea Mitaa yote kuangalia utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi amesema hadi leo viwanja milioni 1.9 vilitakiwa viwe vimepimwa lakini 833,956 tu ndiyo vimepimwa huku hati miliki zilizotolewa ni 87,387.
Aidha, ameagiza ndani ya muda mfupi vyote viwe vimepimwa na hati zitolewe kulingana na idadi ya viwanja.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze, ameeleza mpaka Julai mwaka huu, Kampuni 163 za upimaji na upangaji zinashiriki urasimishaji makazi yasiyopangwa katika mikoa 26 ndani ya Halmashauri 158 katika mitaa yenye urasimishaji 1651.
Na SELINA MATHEW, Dodoma