WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima, amewataka watendaji wanaohusika na mnyororo wa ugavi wa dawa na vifaa tiba kuwa wazalendo, wawajibikaji na wawazi ili kudhibiti upotevu wa dawa.
Pia alisema ili kuboresha huduma za upatikanaji wa dawa nchini, serikali imejenga viwanda vipya 18 vinavyozalisha vifaa tiba ambapo lengo la serikali hadi kufikia mwaka 2030 kuwa na uwezo wa kuzalisha dawa kwa asilimia 50 kutoka 80 iliyopo sasa.
Dk. Gwajima aliyasema hayo Dar es Salaam, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili udhibiti wa upotevu wa dawa nchini, kilichowajumuisha wadau wanaohusika na mnyororo wa ugavi wa dawa, wakiwemo Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari ya Dawa (MSD) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
“Suala la upatikanaji wa dawa siyo ajenda ya bajeti pekee, bali ni ajenda ya uwajibikaji wa kizalendo na nidhamu thabiti ya uongozi kwenye usimamizi sehemu ya kazi tukiyatafsiri hayo kazi yetu itakuwa nyepesi,” alisema.
Pia Dk. Gwajima alitoa agizo kwa wadau wa mnyororo wa ugavi wa dawa kuanza utaratibu wa kutumia kadi ya alama ‘Scole Card’ inayotoa mchanganuo wa matumizi ya dawa ili kuonyesha namna zilivyotumika.
Aidha, aliwaagiza wadau kuhakikisha kikao watakachokaa kinazaa matunda ya kutambua ni maeneo gani yenye mapungufu hadi kusababaisha upotevu wa dawa ili yafanyiwe kazi.
Mfamasia Mkuu wa Serikali Dudi Msami,alisema uzalishaji wa dawa kupitia viwanda vipya 18, vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, vingine vinaendelea na majaribio huku wawekezaji wengi wakiendelea kujitokeza.
Msami alivitaja baadhi ya viwanda hivyo ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha barakoa kilichopo Kigamboni, Dar es Salaam.
Pia alisema kiwanda kingine kipo Makambako eneo la Idofi Mkoani Iringa, ambacho kitafanikisha asilimia 100 ya upatikanaji wa dawa. Malighafi mbalimbali zimeanza kutumika ikiwemo mapipa 500 yamepelekwa.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Rose Shija, alisema Shirika hilo linaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono maazimio ambayo yatapitishwa katika kikao kazi hicho.
Pia alisema WHO ipo tayari kufanya kazi na wadau wote katika sekta ya afya nchini, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD Christopher Kamugisha alisema wataendelea kutekeleza sera na miongozo inayotolewa na serikali ili kufanikisha upatikanaji wa dawa nchini.
Pia Kamugisha aliiomba kuwepo na uwazi na uwajibikaji katika utolewaji taarifa ili kuzifanyia kazi kwa pamoja.
Na IRENE MWASOMOLA