WATUMISHI wa Kampuni ya simu za mkononi ya Halotel, wameadhimisha miaka 6 ya huduma nchini kwa kutoa msaada wa mahitaji kwa watoto wenye changamoto ya vichwa vikubwa, mgongowazi na wazazi waliolazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).
Msaada huo umejumuisha dawa na mahitaji muhimu ya kibinadamu, ambayo yatawawezesha wagonjwa hao kuimarisha afya zao pindi wawapo wodini wakisubiri kupatiwa matibabu ambayo ni kwa njia ya upasuaji .
Akizungumza katika makabidhiano hospitalini hapo, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Mawasiliano Halotel, Sakina Makabu na Afisa Mahusiano ya nje ya kampuni hiyo, Yassir Matsawily, wamesema katika kuhakikisha wanasaidia sekta ya afya nchini ni vyema kuendeleza utamaduni huo wa kuwaona wagonjwa.
“Utaratibu huu ni sehemu ya kuonyesha upendo na kuwajali kutokana na kutambua thamani yao katika jamii ya Watanzania,” amesema Yassir.
Kadhalika ameongeza: “Tunatambua changamoto mbalimbali ambazo ziko katika kuwapa matibabu watoto wenye matatizo ya kiafya ya vichwa vikubwa na mgongowazi wawapo wodini wakisubiri kupatiwa matibabu ya upasuaji.

Hivyo katika kujali na kutambua thamani ya Afya zao, tumeona ni vyema kuwaletea mahitaji haya muhimu ya kuimarisha afya zao.”
Akizungumza baada ya kukabidhiwa msaada huo kwa niaba ya wazazi wengine wodini hapo, Rose Vincent, amesema wanajisikia faraja kukumbukwa na kampuni hiyo na kupokea msaada huo kutoka kwao .
“Tumefarijika sana na tunaomba waendelee na moyo huo huo wa kusaidia jamii ya Watanzania,” amesema Vincent.
Kwa upande wa uongozi wa MOI, Ofisa Uhusiano Patrick Mvungi, amesema ni faraja kupokea msaada huu kutoka kampuni ya simu ya Halotel na wafanyakazi wake, hali inayoonesha kuthamini Afya za watoto wagonjwa hao.
“Hii ni hatua mpya na kubwa na imekuwa endelevu kwetu sisi katika kuimarisha ushirikiano wetu na Halotel kwa kiwango cha juu, hasa katika kuboresha sekta ya afya kwa ujumla,” amesema Mvungi.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, hadi sasa imepiga hatua kubwa katika kusambaza huduma za Mawasiliano na kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu nchi nzima.
Kampuni hiyo imekuwa ikijihusisha na kujali jamii ya Watanzania kwa nyanja mbalimbali ikiwamo kuboresha sekta ya afya, elimu kama moja ya vipaumbele vyake kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya Watanzania na taifa kwa ujumla.
Na WILLIAM SHECHAMBO