SERIKALI chini ya Rais Samia Suluhu Hassan Imetenga kiasi cha sh trilioni 1.1 kwa Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Fedha hizo zitatumika kutekeleza vipaumbele 16 vya afya, ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania itakuwa na Hospitali Maalumu ya Mama na Mtoto.
Katika fedha hizo, Serikali inatarajia kutumia sh. bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kisha kusambazwa katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya.
Akiwasilisha bungeni, hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, amesema wizara itaendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha huduma za afya nchini zinawafikia Watanzania walio wengi hususan wenye kipato cha chini.
“Kipekee nimpongeze Rais Samia kwa uongozi wake imara na kwa dhamira, maono na uthubutu wake, ambao umekuwa dira sahihi inayoongoza utendaji wangu katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.
“Ni dhahiri katika kipindi cha uongozi wake Watanzania wameshuhudia kasi kubwa ya uimarishaji na utoaji wa huduma bora za afya nchini, hususan ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya katika halmashauri na mikoa yote nchini, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za rufani za mikoa, kanda na Taifa,” alieleza.
VIPAUMBELE 16 VYA WIZARA
Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini (CCM) alisema ili kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa katika mwaka wa fedha 2022/2023, wizara imekadiria kutumia kiasi cha sh. trilioni 1.1 kutekeleza majukumu yake ya uendeshaji wa ofisi na miradi wa maendeleo.
Alisema wizara imepanga kununua, kutunza, kusambaza na kutoa chanjo kwa watoto nchini, ambapo sh. bilioni 74.4 zimetengwa na kujenga hospitali maalumu ya Mama na Mtoto jijini Dodoma kuimarisha huduma za tiba kwa magonjwa ya wanawake na watoto ambapo sh. bilioni 10 kimetengwa.
Waziri Ummy alisema sh. bilioni 23.36 kimetengwa kwa ajili ya kujenga vyumba vya huduma za watoto wachanga katika hospitali 100 za wilaya, kuwajengea uwezo watoa huduma kuwa na stadi, weledi, tabia bora katika kutoa huduma za mama na mtoto, kujenga, kuweka vifaa na watumishi wenye weledi katika wodi za wagonjwa wanaohitajai uangalizi maalumu (ICU) za wazazi katika hospitali za kanda na mikoa.
Alitaja kipaumbele cha tatu ni kununua dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuzisambaza katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya, serikali imetenga sh. bilioni 200, kazi ya ukamilishaji ujenzi wa hospitali tano za rufani za mikoa ya Katavi, Geita, Njombe, Songwe na Simiyu, zimetengwa sh. bilioni 18.6.
“Eneo lingine ni kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya tatu za rufani za mikoa ya Shinyanga, Singida na Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Mara) ambapo sh. bilioni 26 zimetengwa.
Kuboresha huduma za matibabu ya ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na za kanda kwa kuimarisha miundombinu na ununuzi wa vifaa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), hospitali za rufani za kanda za Chato, Mtwara, KCMC, Bugando, Mbeya na kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Magharibi, uimarishaji wa Hospitali Teule ya Ukerewe zimetengwa sh. bilioni 16.9
Aliongeza kuwa: “Kuendelea na ujenzi wa wodi ya wagonjwa binafsi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimetengwa sh. bilioni nne, kuanza ujenzi wa jengo la kutolea huduma za uchunguzi na tiba ya saratani, ikiwemo huduma ya mionzi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma ambapo zimetengwa sh. bilioni 10.”
Ummy alikitaja kipaumbele cha kingine ni kukamilisha upanuzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika hospitali nane za rufani za mikoa ambayo mikataba yake bado inaendelea.
Alizitaja hospitali hizo kuwa ni Ligula (Mtwara) Tumbi (Pwani), Bombo (Tanga), Kagera, Maweni (Kigoma), Kitete (Tabora), Sekou – Toure (Mwanza) na Mawenzi (Kilimanjaro) ambapo zimetengwa sh. bilioni 13.6.
Waziri huyo alitaja kipaumbele cha 10 ni kuendelea na ujenzi wa hospitali mbili mpya za mikoa ya Ruvuma na Sokoine (Lindi) ambapo kiasi cha sh. bilioni 2 zimetengwa huku shughuli ya kuwezesha mafunzo ya ubingwa bobezi nje ya nchi nazo zikitarajia kufanyika ambapo sh. bilioni tatu zimetengwa.
Vipaumbele vingine ni kugharamia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi tarajali (sh. bilioni 65), kuimarisha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza (sh. bilioni 12.6), kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (sh. bilioni 26.6), kusimamia utekelezaji Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (sh. bilioni 14.8), huku kipaumbele cha 16 kikiwa kutekeleza afua mbalimbali za afya ambapo sh. bilioni 57.4 zimetengwa.
AJIRA MPYA
Ummy alisema pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya afya kutokana na upungufu wa rasilimali watu, wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kupunguza pengo kati ya upatikanaji wa watumishi ikilinganishwa na mahitaji halisi.
“Katika kufikia azma hiyo, wizara imeendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tunamshukuru Rais Samia kwa kutoa kibali cha ajira mpya kwa wataalamu wa afya ambapo kwa mwaka 2022/2023 zimetengwa nafasi 10,285 za ajira,” alisisitiza.
MAOMBI YA FEDHA
Waziri Ummy aliliomba Bunge kuidhinisha sh. trilioni 1,109,421,722,000 ili kuweza kutekeleza malengo iliyojiwekea ambapo katika mwaka huo wa fedha, wizara imepanga kutumia kiasi cha sh. bilioni 554.2 kwa matumizi ya kawaida sawa na asilimia 50 ya bajeti tengwa, huku sh. bilioni 331.5 mishahara na sh. bilioni 222.7 kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Kuhusu miradi ya maendeleo, alisema wizara yake inakadiria kutumia sh. bilioni 555.1 kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 50 ya bajeti tengwa. Kati ya hizo, fedha za ndani ni sh. bilioni 410.2 na fedha za nje ni sh. bilioni 144.8.
“Katika mwaka wa fedha 2022/2023, wizara na taasisi zilizo chini yake imekadiria kukusanya kiasi cha sh. bilioni 619.5, kati ya fedha hizo, sh. bilioni 140.8 zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya ndani makao makuu ya wizara, sh. bilioni 85.7 zitakusanywa katika hospitali za rufani za mikoa na sh. bilioni 392.9 zitakusanywa kutoka mashirika yaliyo chini ya wizara.
Alihitimisha kuwa: “Makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na makadirio ya mwaka 2021/2022 ambayo yalikuwa sh. bilioni 507.2.”
KAMATI YASISITIZA MATUMIZI DAWA ASILI
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo, alisema kamati inaishauri serikali iwatambue watoa huduma za tiba asilia kwa kuwapa ithibati ili kuwahakikishia usalama wa afya zao wananchi wanapotumia huduma hizo.
Pia, alisema kamati hiyo inaishauri serikali kuweka utaratibu wa usambazaji wa tiba hizo asilia kama sehemu ya matibabu baada ya kupata ithibati ya matumizi yake.
“Ili kuepuka uwepo wa watoa huduma wasio waaminifu, kamati inashauri wizara iwasajili watoa huduma hao na dawa zao ambazo zimethibitika zinatibu magonjwa mbalimbali.
Aidha, serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu tiba asili na tiba mbadala ambazo hazina madhara kwa watumiaji,” alisisitiza.
NA MUSSA YUSUPH, DODOMA