RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wameamua kufanya mazungumzo na wamiliki wa hoteli ambazo wamefikia watalii kutoka Ukraine ili waendelee kuwepo kisiwani hapo.
Amesema watalii 900 kutoka Ukraine walifika Zanzibar kufanya shughuli za kitalii na sasa wanashindwa kurudi nchini mwao kutokana na vita inayoendelea baina ya nchi yao na Russia.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Mjini Zanzibar, alipozungumza na waandishi wa habari na wahariri ikiwa ni utaratibu wake wa kukutana na vyombo mbalimbali vya kila mwisho wa mwezi.
Amesema watalii hao waliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iwapatie hifadhi kwa kipindi hiki ambacho nchi yao ina machafuko na hawana fedha kwa sasa za kuendelea kulipia hoteli.
Ameongeza kuwa Zanzibar ni moja ya nchi ambayo imekuwa ikipokea wageni wengi kutoka Ukraine ambao wanakuja kutalii katika visiwa vya Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Lela Mohammed Mussa, alisema watalii kutoka Ukraine ni soko kubwa kwa kipindi kirefu.
Lela alisema wakati vita vinatokea baina ya Ukraine na Russia, watalii hao walikuwepo visiwani hapo na wengine walimaliza muda wao wa kuwa nchini, hivyo serikali imekubali waendelee kubaki Zanzibar.
Aliwashukuru wamiliki wa hoteli kuwa mstari wa mbele kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, kutoa taarifa ya wageni wote wako wapi na kujua lini waliingia wageni hao.
Lela alisema waliwasiliana na Balozi wa Ukraine ambaye yupo nchini Kenya, ambapo kwa mujibu wa balozi huyo alisema wao wana mpango wa kuwachukua raia wao kuwahamishia nchi ya jirani ikiwemo Poland.
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMMED, ZANZIBAR