MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, amewashukia vikali watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuandika taarifa za uongo na upotoshaji, badala yake watumie nguvu hiyo katika kushirikiana ili kufichua wahalifu.
Alisema baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii hawajui maana ya uvunjifu wa amani na nchi ikiiingia katika matatizo hali itakuwaje.
IGP Sirro, aliyasema hayo, Kurasini Jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari baada ya hafla ya kuwaaga Makamishina wa Jeshi la Polisi, Robert Boaz na Valentino Mlowola katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA).
“Nilikuwa naangalia katika mitandao, baadhi yao hawajui maana ya uvunjifu wa amani, hawajui nchi ikiingia katika matatizo hali inakuwaje, wangejua wasingeweza kuandika mambo ya uongo.
“Mtu anatengeneza jambo katika mtandao, sijui kwa faida ya nani, amani ikipotea kuirudisha ni tabu, wale wanaokomalia mitandao zungumzeni mambo ya ukweli,” alisema.
HAKI ZA WANANCHI NA KAZI ZA POLISI
Aidha, IGP Sirro alisema jeshi hilo halipo kwa ajili ya kumuonea mtu, isipokuwa kutenda haki na kuwashughulikia wahalifu.
“Sisi hatupo kwa ajili ya kumuonea mtu, tupo kutenda haki, wewe kama unachukua bunduki unategemea nini, tena bunduki ya kijeshi unategemea nini wewe, ukiwa na bunduki ukiniwahi sawa, nikikuwahi safi, ujue askari na yeye ni binadamu na anapenda kuokoa maisha yake,” alisema.
MWILI WA HAMZA NA MAKOSA MENGINE
Pia, IGP Sirro alisema mwili wa aliyefanya mauji ya askari watatu, Hamza Mohamed, bado upo mikononi mwa Jeshi la Polisi kwani wanasubiriwa ndugu zake.
Kama wasipotokea Jeshi la Polisi litaukabidhi kwa Halmashauri.
Aliwataka wananchi hasa wazazi kutowaficha watoto wao ambao ni wahalifu, kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara kwake na familia kwa ujumla.
Aidha, aliongeza kuwa makosa yanayosumbua kwasasa ni udhalilishaji vitendo vya kubaka na udhalilishaji pamoja na madawa ya kulevya.
BOAZ AZUNGUMZA
Kwa upande wake, Kamishina Boaz alitoa rai kwa askari waliobakia kazini kuwa na weledi, upendo, uadilifu na nidhamu katika kuwatumikia wananchi.
Aliomba serikali kuwekeza katika teknolojia na vifaa kwa sababu uwanda wa vitendo vya uhalifu unabadilika badilika.
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, kazi ya polisi ni ngumu, ina changamoto nyingi, nashukuru nimefanya kazi na wenzangu kwa moyo mmoja na hadi naondoka jeshini, nashukuru nchi iko salama,” alisema.
Na IRENE MWASOMOLA