Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameupongeza utayari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika utekelyezaji wa milango yake ya maendeleo.
Dk. Mwinyi amesema hayo, Ikulu Zanzibar katika mazunguzo kati yake na Balozi wa Italia nchini, Marco Lombardi, Ikulu Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alipongeza azma ya Italia kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo ya utalii, ambapo nchi hiyo ni mdau mkubwa.
Dk. Mwinyi alisema Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikinufaika kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya wawekezaji na wageni kutoka Italia.
Aidha, Dk. Mwinyi alimuahidi Balozi Lombardi SMZ itaendelea kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha wawekezaji na wageni wanaotoka nchi hiyo na nyingine duniani, wanatekeleza shughuli zao katika mazingira yanayokidhi matarajio yao.
Dk. Mwinyi aliipongeza azma ya Italia kuongeza huduma za usafiri wa anga kwa kuleta ndege kutoka kampuni kubwa za nchi hiyo ambazo zitafanya safari zake moja kwa moja kati ya Zanzibar na Italia.
Pamoja na hayo, Dk. Mwinyi alimweleza Balozi Lombardi kuwa bado Zanzibar ina fursa mbalimbali ambazo wawekezaji wa nchi hiyo wanakaribishwa kuzitumia ikiwemo kuendeleza sekta za uchumi wa buluu, ujenzi wa nyumba za kisasa na majengo ya biashara, kuendeleza ujenzi wa viwanda, kuwawezesha wajasiriamali na kuliimarisha zao la mwani.
Awali Balozi Lombardi alimweleza Dk. Mwinyi kuwa serikali ya Italia inaziona juhudi zinazochukuliwa na SMZ, hivyo iko tayari kuendelea kuziunga mkono.
Balozi Lombardi alimuhakikishia Dk. Mwinyi Italia itaendelea kushirikiana na SMZ katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika nchini.
Katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Balozi Lombardi alimweleza Rais Dk. Mwinyi azma ya ubalozi huo kufanya kongamano kubwa la biashara Septemba mwaka huu, mjini Zanzibar, ili kujadili fursa mbalimbali za uchumi zilizopo.
Aidha, alimweleza Rais Mwinyi azma ya kampuni kubwa za nchi hiyo kufanya safari zake za ndege moja kwa moja.
Na MWANDISHI WETU, Zanzibar