WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, amesema tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za muungano kupitia vikao vya kamati ya pamoja ya Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2006, hoja 25 zimejadiliwa na hadi sasa hoja 18 zinapatikana ufumbuzi.
Alitoa kauli hiyo, mjini Dodoma, wakati akianisha mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Uhuru ikiwemo kusimamia utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa ufanisi mkubwa, hali iliyowezesha kuimarika kwa Utaifa, Umoja, Amani na Utulivu na hali ya maisha ya wananchi katika nyanja za kiuchumi.
Waziri huyo alisema, mambo 22 ya Muungano kama yalivyoanishwa katika nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 yanatekelezwa na Wizara na taasisi zenye dhamana ya kusimamia mambo hayo.
Alisema mambo hayo kuwa yanahusu Katiba, Bunge na Utawala Bora, Uchumi, Fedha na Biashara, Ulinzi na Usalama, Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa, Usafiri na Usafirishaji, Utabiri wa Hali ya Hewa na Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Waziri Jafo alisema katika kipindi cha miaka 60, Serikali zote mbili zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa mambo hayo kwa ufanisi mkubwa na mafanikio yanaonekana katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya kiuchumi, alisema mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kiutawala yamefanyika kwa lengo la kufufua uchumi, kuimarisha utendaji kazi serikalini na kukuza demokrasia na utawala bora.
“Utekelezaji wa programu mbalimbali za mageuzi ya kiuchumi na mipango yakupunguza umaskini na kukuza imezaa matunda tunayojivunia leo,” alisema Jafo na kuongeza kuwa nchi imeimarisha miundombinu ya barabara, usafiri wa anga, usafiri wa majini na huduma za jamii katika pande zote za Muungano.
Kuhusu, mafanikio ya kijamii, Waziri Jafo alisema uwepo wa Utaifa na Umoja, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeunganisha watu wa nchi mbili na kuunda taifa moja la Tanzania.
Alisema historia ya uhusiano wa kidugu wa muda mrefu baina ya watu wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa chachu muhimu ya kuibua hisia za utaifa na hivyo kupanda mbegu ya utaifa.
“Watanzania kwa pamoja wanajivunia utaifa wao popote wanapokuwa, lugha adhimu ya taifa, kiswahili inayozungumzwa takribani na watanzania wote imechangia kuwaunganisha na kukuza utaifa,” alisema.
Kuhusu mazingira, alisema serikali imefanikiwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na vifungashio na mifuko ya plastiki kwa kupiga marufuku uingizaji nchini, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya vifungashio hivyo kuanzia Machi Mosi, 2017 na kufanikisha kuondoa matumizi ya viroba.
“Kutokana na katazo hilo wajasiriamali na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali vimeanzishwa na vinatengeneza mifuko ya karatasi, nguo na vikapu ambapo hadi sasa vikundi 2,772 vinavyotengeneza mifuko mbadala vimeanzishwa huku ikikadiriwa takribani ajira 50,000 zinatokana na usambazaji wa mifuko mbadala,” alisema.
Aidha, alisema ofisi hiyo imeendelea na kampeni ya upandaji miti kwa lengo la kurejesha uoto wa asili na kupunguza hali ya kuenea kwa jangwa na ukame ambapokila Halmashauri ya wilaya imeelekezwa kupanda miti milioni 1.5 Kila mwaka.
Pia, alisema hadi kufikia Mei mwaka 2020, takribani miti 608,594 464 ilipandwa katika mikoa 26 katika halmashauri zote na baada ya tathimini asilimia 62.8 ya miti iliyopandwa ndiyo iliyopona.
“Mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka 60 ya uhuru yametokana na jamii yenye umoja, mshikamano na isiyo na ubaguzi. Watu wa pande mbili za muungano wanaishi na wanafanya kazi zao za kujiletea maendeleo katika sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kubughudhiwa,” alisema.
Na SELINA MATHEW, Dodoma