WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, ametoa onyo kwa watu wanaovamia mito na mabonde na kuchimba mchanga bila vibali na atakayekamatwa atakuwa mfano kwa wengine.
Onyo hilo amelitoa Ulongoni, Dar es Salaam, katika majumuisho ya ziara yake ya kukagua mito na mabonde mbalimbali ya jiji hilo na kuangalia kazi iliyofanywa na kikosi kazi cha kudhibiti mmomonyoko katika mito.
Kikosi kazi hicho kinawahusisha maofisa wa Polisi, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoa wa Dar es Salaam, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na maofisa kutoka Manispaa za Dar es Salaam.
Jafo amesema serikali inatumia gharama kubwa kutengeneza kingo za mito ili kuhakikisha watu walio jirani na mabonde hayo wanakuwa salama, hivyo kuendelea kuchimba mchanga ni kuhatarisha maisha yao.
Ameeleza kumekuwa na changamoto kubwa ya kutunza mito na mafuriko yamekuwa yakitokea na sababu kubwa ikielezwa ni uchimbaji wa mchanga katika maeneo hayo.
“Watu wote wanaovamia mito na kuchimba mchanga bila vibali na kusababisha mmomonyoko na kuhatarisha maisha ya watu na watakaokiuka agizo langu watachukuliwa hatua kali na hii itakuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” amesema.
Amebainisha kuwa, Wizara yake iliunda kikosi kazi maalumu cha kusimamia usafishaji wa mito, ambacho alikipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika kwa kuwa kimefanikiwa kusafisha mito hiyo kwa urefu wa kilomita 47.
Jafo ameahidi kwamba atahakikisha kikosi kazi hicho kinawezeshwa kifedha ili kazi nzuri waliyoifanya inaendelea katika mikoa mbalimbali na kuwataka wananchi waheshimu sheria za nchi na kuachana na uvamizi wa mito na mabonde.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeifanya ajenda ya mazingira kuwa ni endelevu, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi wa mazingira ya vizazi vijavyo kwa kuwa serikali inatumia gharama kubwa kutengeneza miundombinu inapoharibiwa.
Mjumbe wa kikosi kazi hicho, Angela Kibiriti kutoka Jeshi la Polisi, amesema kikosi kazi hicho kimefanikiwa kutoa elimu ya athari za kukaa jirani na mito na kuwa walinzi wa watu wanaochimba mchanga.
Amesema kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ili wawe na uelewa wa pamoja ili serikali ijipange kuwasaidia ili mafuriko yakija wawe salama kwa kuwa nyumba nyingi zimebomoka kutokana na vitendo vya baadhi ya watu wanaovamia mito kuchimba mchanga.
Na Mwandishi Wetu