WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Sulemani Jafo, amewataka wa kazi wa mkoa wa Mara kujikita zaidi katika kilimo cha alizeti huku zao hilo likisadikiwa kuweza kupunguza gharama za ununuaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Hayo amesema katika maonyesho ya sita ya kilimo mseto kwa kipato na uhifadhi wa Mazingira mkoani humo.
Jafo amesisitiza uwekezaji wa kilimo cha zao hilo na kuwataka wanamara kutambua thamani ya zao hilo ikiwemo kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Zao hili ni zao muhimu ambalo tukielekeza nguvu zetu tunaweza kuisaidia serikali katika kupunguza gharama za hapa na pale”amesema.
Aidha, Jafo amesisitiza suala la upandaji miti kwa kila halmashauri ilikwendana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Kwa upande wake Meneja wa VI Agroforestry nchini, Kent Larsson, amesema kilimo mseto ni kilimo kinachopambana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoathiri kilimo.
Amesema VI Agroforestry mwaka huu wamejikita zaidi katika kutafuta mchango wa sera ya kilimo mseto kwenye haki ya chakula na jinsi ukatili wa kijinsia unavyochangia katika ukosefu wa chakula.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi, amesema mpango wa mkoa ni kupanda miti zaidi ya million 9 ilikulinda Mazingira na kila Kijiji kihakikishe kinakuwa na msitu wake kwa ajili ya matumizi yao binafsi.
“Watu wamejisahau kabisa unakuta mtu anakata mti bila kujali hadi kunapelekea baadhi ya maeneo kuwa jangwa” amesema RC Hapi.
Na Naziah Kombo, Mara.